Licha ya serikali ya mapinduzi zanzibar kusema elimu bure lakini bado wazazi wanaambiwa wachangie ili kuunga mkono serikali.

Wazazi na walezi wa wanafunzi wanaosoma katika skuli za serikali wametakuwa kuchangia huduma za elimu ili kuunga mkono juhudi za serikali za kuimarisha sekta ya elimu nchini.

Akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa madarasa ya skuli ya Bububu sekondari, Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Ayoub Mohammed Mahmoud amesema azma ya serikali ya Zanzibar ya kuondoa michango kwa wanafunzi wa elimu ya msingi miaka miwili iliyopita na kwa elimu ya sekondari baadae mwaka huu hakuondoi wajibu wa jamii kuchangia sekta hiyo ili kutia matokeo yaliyo bora zaidi.

Amesema katika kuimarisha ubora wa elimu serikali inaifanyia mapitio ya sera ya elimu Zanzibar pamoja na kuweka miundombinu itakayowezesha kupunguza changamoto mbali mbali zinazoikabili sekta ya elimu Zanzibar hivyo jamii inapaswa kuendeleza utamaduni wa kusaidia skuli na wanafunzi ili kufikia malengo yao.

Aidha amewaasa wanafunzi mkoani humo kuzingatia masomo yao na kujiepusha na mambo yanayopelekea kutofanya vyema katika matokeo ya mitihani yao ya mitihani.

Amesema kwa miaka miwili iliyopita skuli za mkoa huo zimekuwa zikipata matokeo mabaya katika mitihani ya kidato cha nne na sita jambo ambalo linapaswa kupangiwa mkakati wa kujiondoa na hali hiyo.

Akisoma risala kwa niaba ya walimu, wanafunzi na kamati ya maendeleo ya skuli hiyo mwalimu Bimkubwa Abdulrahman Hemed amesema skuli hiyo inakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ya uhaba wa madarasa ya kusomea na kufanyia mazoezi ya vitendo wakati wa mitihani jambo ambalo linaloathiri mwenendo wa kitaalamu na kumuomba mkuu huyo wa mkoa kusaidia kutatua changamoto hiyo.

Akijibu risala hiyo mkuu wa mkoa amesema ofisi yake kupitia kampeni ya Mimi na Wewe itachangia ujenzi wa madarasa na ukumbi wa mitihani kwa kushirikiana na manispaa ya Magharibi ‘A’ kwa kutoa matofali 1,500 na mifuko 50 ya saruji na kuwataka wadau wengine kuchangia ujenzi huo.

Zanzibar24.

Comments