Katika hali ambayo, maandamano na malalamiko ya kupinga kuendelea kushikiliwa kizuizini Sheikh Ibrahim Zakzaky, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yanaendelea kushuhudiwa katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika, polisi na vikosi vya usalama vya Nigeria vimetumia risasi hai na gesi za kutoa machozi kuwatawanya wafuasi wa mwanaharakati huyo wa Kiislamu.
Vyombo vya habari vimetangaza kuwa, baadhi ya barabara za Abuja mji mkuu wa Nigeria zimejaa mikebe ya mabomu ya gesi ya kutoa machozi ambayo imekuwa ikitumiwa na vyombo vya usalama kuwatawanya waandamanaji wanaotaka kuachiliwa huru Sheikh Zakzaky. Aidha baadhi ya ripoti zinasema kwamba, vikosi hivyo vya usalama vimekuwa vikiwakamata kiholela raia hao.
Ibrahim Mussa, afisa habari wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amesema kuwa, polisi na vikosi vya usalama vya nchi hiyo daima vimekuwa vikiwakwaza wanachama wa harakati hiyo. Ameongeza kuwa, polisi imekuwa ikiamiliana kwa mabavu na mikusanyiko ya amani ya wananchi huku ikitumia mabomu ya gesi ya kutoa machozi na kwamba, idadi kadhaa ya wanachama wa harakati hiyo wametiwa mbaroni huku mmoja akiuawa.
Hata hivyo lililo wazi ni kuwa, hujuma na mashambulio ya vikosi vya usalama dhidi ya waandamanaji hao hayajawafanya wasalimu amri, bali wameendelea kudai matakwa yao yatekelezwe kubwa zaidi likiwa ni kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe.
Ibrahim Mussa afisa habari wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria amebainisha kwamba, vyombo vya usalama vya nchi hiyo vikiwa na lengo la kushadidisha chuki dhidi ya Waislamu vimeendesha propaganda kubwa dhidi ya harakati hiyo na kumtendea dhulma kubwa Sheikh Zakzaky pamoja na mkewe.
Amesema, viongozi wa Nigeria hususan Rais Muhamadu Buhari wanapaswa kumuachilia huru Sherikh Zakzaky, mkewe pamoja na wanachama wengine wa harakati hiyo wanaoshikiliwa kinyume cha sheria.
Wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo inajulikana kama kundi la Kishia, wameapa kuendelea na maandamano na malalamiko yao hadi Sheikh Zakzkay atakapoachiliwa huru.
Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa na mke wake walitekwa nyara na Jeshi la Nigeria mwezi Disemba mwaka 2015 wakati askari walipovamia kituo chake cha kidini huko katika mji wa Zaria jimboni Kaduna.
Tokea wakati huo Sheikh Zakzaky na mkewe wamekuwa wakizuiliwa katika mojawapo ya vituo vya kijeshi vya nchi hiyo bila kufunguliwa mashtaka.
Uvamizi huo ulijiri baada ya Jeshi la Nigeria kudai kuwa wafuasi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria walikuwa na njama ya kutaka kumuua mkuu wa jeshi hilo, madai ambayo yalikanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Inakadiriwa kuwa Waislamu 1000 wasio na hatia waliuawa katika tukio hilo.
Malalamiko na maandamano ya kutaka kuachiliwa huru Sheikh Ibrahim Zakzaky, Katibu Mkuu wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yanaendelea katika hali ambayo, kila siku kumekuwa kukiripotiwa habari za kuzidi kuwa mbaya afya ya mwanaharakati mhuyo.
Kinachowashangaza wengi, ni hatua ya serikali ya Nigeria ya kuendelea kumshikilia Sheikh Ibrahim Zakzaky, licha ya Disemba mwaka 2016 mahakama ya nchi hiyo kutoa amri ya kuachiliwa huru kiongozi huyo wa Kiislamu.
chanzo:parstoday.
Comments