Alisema tabia ya kuendelea kuyaachia mashirika ya kigeni kutoa huduma
kwa kampuni zinazosafirisha watalii katika mataifa ya Afrika inaweza
kuviza azma ya Afrika katika kuitegemea sekta hiyo kiuchumi.
Alitoa kauli hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu
wa Pili wa Rais wa Zanzibar , Balozi Seif Ali Iddi, wakati akiufungua
mkutano wa saba wa Shirikisho la Mashirika ya Ndege ya Afrika (AFRAA)
unaofanyika hoteli ya Zanzibar Beach Resort Mazizini.
Alisema usafiri wa anga na utalii ni sekta muhimu kimataifa zinazokua
kwa haraka kiuchumi na kwenda sambamba katika uendeshaji wake jambo
ambalo mataifa ya Afrika kupitia AFRAA, hayana budi kuhakikisha sekta
hizo zinaendelea kujengewa miundombinu madhubuti.
Alisema baraza la usafiri na utalii ulimwenguni limetoa takwimu
zinazoonyesha na kuthibitisha kuimarika kiuchumi kwa sekta hizo mbili
katika kipindi cha 2018.
Alisema usafiri wa anga unaowaunganisha watalii wanaotembelea maeneo
mbali mbali duniani zinatarajiwa kuongeza mapato ya nchi husika
sambamba na fursa za ajira.
Aliitolea mfano Zanzibar ilivyopiga hatua kubwa kimaendeleo na uchumi
katika sekta ya utali kutokana na kuimarika kwa huduma za usafiri wa
anga zinazowaunganisha watalii kutoka pambe mbali mbali duniani.
Aliwaeleza wajumbe hao kwamba idadi ya watalii walioingia Zanzibar
433,166 mwaka 2017 ikilinganishwa na watalii 479,242 kwa mwaka 2016.
Alifahamisha kwamba wakati Watalii wanaoingia Zanzibar wakiongezeka
na kufikia asilimia 14.2 ongezeko hilo linatarajiwa kufikia watalii
500,000 mwaka 2020.
“Nimefarajika kutokana na uamuzi wa AFRAA kufanya mkutano wao
Zanzibar jambo ambalo Zanzibar itapata fursa ya kujitangaza kiutalii
kupitia mkutano huo,” alisema.
Alieleza kuwa juhudi zinazoendelea kuchukuliwa na serikali
zinakusudia kuifanya Zanzibar kuwa na hadhi ya juu katika uimarishaji
wa sekta ya utalii kwenye ukanda wa bahari ya Hindi.
chanzo: Zanzibarleo.
Comments