‘Dk. Shein amesimamia utawala bora’.

WATENDAJI mbalimbali serikalini, wameipongeza serikali ya awamu ya saba  chini ya uongozi wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, kwa kusimamia vyema utawala bora.

Hayo waliyasema wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hizi, kuhusu mafanikio ya Dk. Shein, katika kipindi cha miaka saba ya uongozi wake.

Walisema, Dk. Shein ameonesha dhamira ya dhati ya kuimarisha utawala bora kwa kuanzisha taasisi zinazosimamia sekta hiyo na kuzijengea uwezo.

Walisema utawala bora ndio dira ya kuimarisha demokrasia, usawa, uwazi na uwajibikaji kwa wananchi na viongozi  katika ngazi tofauti.

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Khalid Salum Mohammed, alisema ndani ya uongozi wake, Dk. Shein ametunga sheria mpya ya usimamizi wa fedha za umma ikiwa ni sehemu ya kusimamia utawala bora.

Alisema kutokana na jitihada hizo, ukusanyaji mapato umeongezeka na kupunguza utegemezi wa bajeti kuu ya serikali kutoka kwa wafadhili.

Mkurugenzi Idara ya Uratibu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Khalid Abdalla Omar, alisema miongoni mwa mambo mengine muhimu ndani ya miaka saba ya uongozi wa Dk. Shein ni pamoja na kupeleka madaraka kwa wananchi ili waweze kuibua, kupanga, kutekeleza na kutathmini utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo kupitia serikali za mitaa.

Kuhusu udhalilishaji, Ofisa Mipango wa mahakama kuu, Thuwaiba Amour Haji, alisema katika kipindi hicho kesi mbalimbali zilifunguliwa katika mahakama za Unguja na washtakiwa kupewa hukumu.

chanzo: zanzibarleo.

Comments