Aliyedai ni binti wa Lowassa ajipalia makaa polisi.

Uamuzi wa Fatuma Chikawe (31), kujitangaza mbele ya vyombo vya habari kuwa ni mtoto wa Edward Lowassa aliyetelekezwa umemgeuka; sasa anakabiliwa na uwezekano wa kufikishwa mahakamani kwa tuhuma za kumdhalilisha waziri huyo mkuu wa zamani.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa amesema wanamhoji Fatuma kwa kusababisha taharuki katika jamii.
Akizungumza na Mwananchi jana, Mambosasa alisema: “Ni kweli tunamshikilia huyo msichana aliyejitokeza na kudai ni mtoto wa Lowassa. Tunamhoji baada ya kukiri amedanganya, kwa makosa ya kumdhalilisha na kusababisha taharuki kwa jamii.”
Mambosasa alisema wanaendelea na upelelezi na utakapokamilika watamfikisha mahakamani.
Msichana huyo alikuwa miongoni mwa wanawake waliojitokeza katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam iliyotaka kusaidia wanawake waliotelekezewa watoto na wazazi wenzao.
Lakini Fatuma aliibuka katika ofisi hizo akidai kuwa baba yake ni Lowassa na kuwa hajawahi kumuona tangu azaliwe, hivyo alihitaji kuunganishwa naye.
“Namtafuta mzazi wangu, sijawahi kumuona na mama yangu aliniambia kuwa baba yangu ni Edward Lowassa na sasa mimi napata shida. Nahangaika kwa sababu simjui baba yangu,” alisema msichana huyo.
Hata hivyo, Aprili 15 alionekana katika video nyingine iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii akimuomba radhi Lowassa kutokana na kitendo chake kuchukuliwa kisiasa na hivyo kumdhalilisha.
Mara baada ya video ya kwanza kusambaa, mmoja wa watoto wa Lowassa, Fred, aliandika kwenye akaunti yake kuwa familia ya Lowassa haikatai watoto na kueleza kushangazwa na jinsi msichana huyo alivyoshindwa kuwasiliana na ndugu wa familia hiyo aliyosema wako wengi.
Aprili 14, mkuu wa mkoa, Paul Makonda alisema ana majina zaidi ya 100 ya viongozi wakiwamo wa dini na wabunge ambao walitajwa.
Alisema kama hawatamaliza mambo yao kimyakimya watakiona.
Mwananchi.

Comments