Zanzibar yakaza uzi kupambana na ugonjwa wa Malaria.

Meneja Mradi wa kumaliza Malaria Zanzibar  Abdallah Suleiman amesema Licha ya Maradhi ya Malaria  kupungua Nchini lakini kuna baadhi ya maeneo bado maradhi hayo yanaonekana kuwepo kutokana na wananchi kutotumia vyema  Elimu wanayopewa juu ya kutokomeza maradhi hayo.

Akizungumza nje ya Mkutano wa kutathmini Mpango kazi wa mwaka 2017 na kupanga Mpango kazi wa mwaka 2018/20  wa kupambana na maradhi ya Malaria, Meneja huyo amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa katika kutokomeza ugonjwa huo lakini kuna baadhi ya wananchi wanachangia kudumaza mafanikio hayo.

Amesema kitengo cha Malaria kimekuwa kinachukuwa jitihada mbali mbali ikiwemo kupiga dawa majumbani na kugawa vyandarua lakini baadhi ya watu wanakataa kutumia vyandarua kisheria na badala yake wanavitumia kwa mahitaji yasiyostahiki na kusababisha ugonjwa kutopungua katika makaazi yao.

Hata hivyo amesema kitengo cha kukabiliana na malaria nchini kimeandaa utaratibu maaalumu wa kufatilia taarifa za wagonjwa wa maradhi majumbani mwao ili kuweza kuwapatia matibabu wangonjwa watakao bainika na Ugonjwa wa malaria kwa lengo la kuzuia ugonjwa huo kuenea Nchini.

 Awali akifungua Mkutano huo Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhammed amewataka wafanya kazi wa Wizara yaAfya kuendelea kutumia vyema miradi ya maendeleo katika kutoa matibabu bora kwa wagonjwa ili kupunguza matatizo yanayoikabili sekta ya afya ikiwemo uhaba wa vitendelea kazi.

Aidha ametowa wito kwa wafanya kazi kuhakikisha huduma  na elimu ya kujikinga na Maradhi ya Malaria inawafikia walengwa ili kuzuia maradhi hayo kurejea nchi na kuisababishia hasara Serikali.

Nae Mkurugenzi wa Mradi wa Kumaliza Malaria Tanzania Bara Waziri Nyoni amesema hali ya Malaria Tanzania bara hairidhishi ambapo utafiti umeonesha kuwa Maradhi hayo yapo kwa asilimia 7.3.

Mkutano huo umeshirikisha wadau wa sekta ya afya kutoka maeneo ya Zanzibar na nnje ya Zanzibar ili kufanya tathmini ya maambukizi ya Ugonjwa huo pamoja na kuanda mikakati ya kuweza kutokomeza Ugonjwa huo Nchini.
chanzo:Zanzibar 24.

Comments