SMZ yakusudia kupambana na maradhi ya aina hii.

Wizara ya Afya Zanzibar imekusudia kupambana na maradhi yasiyopewa kipaombele ikiwemo kichocho na Minyoo ili  kuondoa hatari kubwa inayoweza kujitokeza kwa wananchi  pindi maradhi hayo yakienea nchini.

Akizugumza na Waandishi wa habari baada ya Mazungumzo na wawakilishi wa Serikali ya China kuhusu kupambana na Maradhi hayo, Waziri wa Afya Zanzibar Hamad Rashid Muhammed amesema  wataungana bega kwa bega na serikali ya China kufanya utafiti utakao wawezesha kukabiliana na maradhi hayo kwani yanaweza kuleta athari kubwa kwa wananchi na kupoteza fedha za serikali pindipo yataenea katika jamii.

Akizungumzia Mradi wa Maradhi yasiyoambukizwaa unaofadhiliwa na Serikali ya China Mkuu wa kitengo cha Maradhi hayo Dk.Fatma Kabole amesema mradi huo utajikita katika utoaji wa dawa za kujikinga na  maradhi hayo.

 Amesema Mradi huo pia umekusudia kumwaga dawa za kuuwa wadudu wanaosambaza maradhi ya kichocho katika maeneo yote yenye kutuwama maji ikiwemo Mwera kwa Unguja na Kitongoji na Wingwi kwa Pemba na kutoa wito kwa wananchi kuwa na tahadhari ya kutumia maji yaliyotuama.

 Aidha Waziri wa Afya nae ametoa wito kwa wafanyakazi wa wizara yake kuendeleza ushirikiano mzuri kwa wadau wa maendeleo wanye malengo ya kuanzisha miradi ya kutoa matibabu kwa wananchi ili waweze kunufaika na huduma za matibabu zinazotolewa.
chanzo: Zanzibar24.

Comments