Sisitizo juu ya ulazima wa kuwasilishwa ICC faili la maangamizi ya kizazi nchini Myanmar.

Sisitizo juu ya ulazima wa kuwasilishwa ICC faili la maangamizi ya kizazi nchini MyanmarKamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametangaza kuwa Baraza Kuu la umoja huo linapasa kuwasilisha kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) faili la jinai zilizofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya.

Zeid Ra'ad al Hussein anasema Waislamu wa  jamii ya Rohingya huko Myanmar wamekabiliwa na maangamizi ya kizazi na ni mahakama ya ICC pekee ndiyo inayoweza kuthibitisha mauaji hayo. 
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa pia ameitaka serikali ya Myanmar iwaruhusu viongozi wa Umoja wa Mataifa kutembelea mkoa wa Rakhine magharibi mwa nchi hiyo ili wachunguze suala la kutokea maangamizi ya kizazi katika mkoa huo wenye wakazi wa Kiislamu. 
Rais zaidi ya elfu sita Waislamu wa jamii ya Rohingya waliuawa, elfu nane kujeruhiwa na wengine karibu milioni moja wamelazimika kuwa wakimbizi tangu Agosti 25 mwaka jana kufuatia mashambulizi yaliyofanywa na jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo mikali dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine.
Hii si mara ya kwanza kuona maafisa wa Umoja wa Mataifa na taasisi nyingine za kimataifa zinatangaza kuwa, yanayofanywa na jeshi na Mabudha hao wenye misimamo ya kufurutu ada wa Myanmar dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya ni maangamizi ya kizazi na jinai za kivita.
Hata hivyo nukta iliyo na umuhimu ni kuwa wale wote wanaodai eti ni watetezi wa haki za binadamu si tu kuwa hawazingatii ripoti hizo, bali kimya chao kimewatia kiburi zaidi watenda jinai huko Myanmar. 
Hii ni katika hali ambao duru za nchi za Magharibi hususan Marekani zimedhidhirisha kikamilifu mienendo yao ya undumakuwili kuhusu masuala ya haki za binadamu kwa kuwaunga mkono wafanya magendo ya madawa ya kulevya kwa hatua yao ya kuanza mchakato wa kufungua faili la kumpelekea katika mahakama za kimataifa Rais Rodrigo Duterte wa Ufilipino ambaye  ameanzisha vita ya pande zote dhidi ya mafia ya mihadarati nchini humo.  
William O. Beeman, mhadhiri na Profesa katika Chuo Kikuu cha Minnesota nchini Marekani anasema kuwa: Myanmar hivi sasa haina faida wala maslahi yoyote ya kistratejia kwa madola makubwa kiuchumi duniani hususan Marekani. Japokuwa kumegunduliwa mafuta kwa mara ya kwanza huko Myanmar, lakini hivi sasa maslahi ya kiuchumi ni machache au hayapo kabisa kwa ajili ya Marekani. 
Kwa msingi huo duru zenye mfungamano na Waislamu wa Rohingya  zinaamini kuwa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) inapasa kuwajibika ipasavyo na kuifikisha serikali ya Myanmar katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai; na wakati huo huo taasisi za kimataifa ziunde tume huru za kuchunguza hali ya Waislamu wa Rohingya katika mkoa wa Rakhine na ziishinikize serikali ya Myanmar ili iafiki suala hilo.  
Nour al Islam, Mkuu wa Taasisi ya Kitaifa ya Arakan amesema kuwa: Tume huru inapasa kuundwa kuchunguza mauaji dhidi ya Waislamu katika mkoa wa Rakhine huko Myanmar. Mashinikizo ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya vijiji vingi na mauaji ya halaiki dhidi ya Waislamu wa kabila la Rohingya huko Myanmar yangali yanaendelea. 
Kwa vyovyote vile, pamoja na kuwa Umoja wa Mataifa umewaarifisha Waislamu wa Rohingya kuwa jamii iliyodhulumika zaidi duniani, lakini hadi sasa umoja huo na taasisi nyingine za kimataifa hazijachukua hatua yoyote ya jadi ya kutambua haki za kiraia za jamii hiyo. 
Hii inamaanisha kuwa, si jambo lililo mbali kukaririwa jinai za jeshi la Myanmar na Mabudha wenye misimamo mikali wa nchi hiyo iwapo Waislamu hao watarejea kwenye makazi yao. 
chanzo:parstoday.

Comments