Simba yaikabili Stand United kibabe.

MASHABIKI wa Yanga huko mitaani wanachekea tumboni baada ya kusikia nyota wa watani zao Simba, Emmanuel Okwi na John Bocco 'Adebayor' kuwa majeruhi na kuamini huenda watarahisishiwa kazi ya kupunguza pengo la pointi baina yao.
Simba inayoongoza msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na alama 45, pointi tano zaidi na ilizonazo Yanga waliopo nafasi ya pili, inatarajiwa kushuka Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam leo Ijumaa kuikarisha Stand United bila nyota wake hao wawili.
Jambo hilo limewafanya Yanga wachekelee wakiamini kasi ya watani zao huenda ikapungua kupitia mchezo wa leo, lakini wakasahau kuwa kwa sasa Simba ipo chini ya makocha wajanja na wenye njaa ya kuona mnyama anabeba ndoo msimu huu.
Kocha Mfaransa Pierre Lachantre na msaidizi wake, Masudi Djuma tangu mapema walishajua itawakosa nyota wake hao wawili waliofunga jumla ya mabao 26 katika ligi ya msimu huu na fasta wakajipanga kibabe kuweka wabadala wa mastraika hao.
Kocha Djuma alikiri ni kweli katika mechi ya leo Okwi hataucheza kabisa kwani bado ana maumivu na hata mazoezi na wenzake alishindwa kuyafanya kujiandaa na mchezo huo, lakini bado anaamini timu yake itaifunga Stand vyovyote vile.
Mrundi huo alisema, hata Bocco aliyefanya mazoezi na wenzake bado hajawa fiti kuweza kushuka uwanjani tangu aumie katika mechi dhidi ya Mwadui, lakini tayari amewaandalia silaha nyingine wapinzani wao ili kupata ushindi.
"Kiu yetu msimu huu ni kubeba taji na kuiletea Simba mafanikio, hivyo hata bila ya nyota hao, bado kuna wachezaji wengine ambao wataibeba timu kupata matokeo mazuri mbele ya Stand," alisema Kocha Djuma.
Djuma bado ina nyota wenye uchu wa kutupia kambani, akiwamo Shiza Kichuya mwenye mabao saba mpaka sasa, Nicholas Gyan aliyeanza kufunga mabao kwa sasa, Mzamiru Yasin na wengine walioisaidia timu yao kufunga mabao 46 hadi sasa.
Hata hivyo Kocha Msaidizi wa Stand, Augustino Malindi alisema kwa ufundi kuelekea mechi hiyo itakayopigwa saa 10 jioni;
"Tumekuja kusaka pointi tatu ambazo ni muhimu, kwani hatupo katika nafasi nzuri, hivyo Simba isitarajie mteremko, hatufungwi tena." Katika mechi ya awali mjini Shinyanga, Stand ililala mabao 2-1.
MGHANA MZUKA
Mshambuliaji Nicholas Gyan limevunja rekodi ya kuichezea Simba mechi 18 bila bao kabla ya kufunga wikiendi iliyopita, alisema bao dhidi ya Mbao limempa mzuka kinoma.
Gyan  aliyesajiliwa msimu huu kutoka Ebusua Dwarfs alifunga bao hilo wakati Simba ikiishindilia Mbao mabao 5-0 kwenye Uwanja wa Taifa na Mghana huyo alisema bao hilo limempa kasi ya kuendelea kufanya vizuri na wana Simba wasubiri waone mambo.
"Kila kitu ni kuweka nia nia yangu ilikuwa kufunga katika mechi moja tu na naimani kuwa unaweza kuwa mwanzo mzuri kwangu katika kufunga na kuwa sehemu ya wachezaji waliofunga magoli kadhaa ndani ya timu," alisema Gyan.

Comments