Serikali yazuia ujenzi Kihinani, Chuini.


KATIKA kuendeleza marufuku ya ujenzi wa makaazi ya kudumu maeneo ya Chuini, Mbuzini hadi Kihinani wialaya ya Magharibi ‘A’ Unguja, serikali imeweka tena mabango yanayoashirika kuendelea kuzuia maeneo hayo kwa shughuli za ujenzi.

Akizungumza na waandishi wahabari waliofika kwenye maeneo hayo, Mkurugenzi wa ardhi katika Kamisheni ya ardhi ambae pia ni Katibu wa bodi ya uhaulishaji ardhi, Said Salmin Ufuzo, alisema uwekaji wa mabango hayo ni utekelezaji wa amri ya serikali kufuatia tangazo lake lililotolewa katika gazeti la serikali toleo nambari 5622 la 1993.

Alisema serikali ilizuia maeneo hayo kisheria na yalitengwa kwa ajili yamatuzi ya serikali.

Aidha, alieleza awali serikali ilifanya uhakiki wa majengo yote yaliyokuwepo kipindi hicho na kuweka ramani ambayo bado ipo kwenye kumbukumbu na kutambulika kisheria.

“Mwaka 2015 serikali ilifanya tena uhakiki na kubaini ongezeko la nyumba na ujezi wa makazi ya kudumu, hivyo serikali kupitia tawala za mikoa ilifanya jitihada za kuweka alama za ‘X’ kwenye nyumba zote zilizojengwa kwenye eneo la serikali lililokatazwa,”alisema.

Naye, Sheha wa shehia ya Chuini, Juma Muhammed Khatib, aliwaomba  wananchi wa shehia hiyo kufuata agizo la serikali kwa kutii amri zote zinazotolewa na serikali kuu.

Aidha aliwaomba  kuwa na utaratibu wa kusoma matangazo yanayowekwa na serikali.
Aidha, aliwataka wananchi waliojenga kimakosa kwenye maeneo yaliyokatazwa waanze kuhama na kuvunja taratibu ili kupisha eneo hilo kwa ajili ya matumizi ya serikali.

Wakizungumza na Zanzibar Leo kwa nyakati tofauti, wananchi wa shehia hizo waliiomba serikali kuwasamehe japo kwa kuwatoza fidia badala ya kuwahamisha ama kuwavunjia kwa vile wametumia gharama kubwa ndani ya miaka 25.

Walisema licha ya ugumu wa maisha unaowakabili wananchi wa Zanzibar, suala la makazi ni muhimu kwao kwa vile wamewekeza kwenye maeneo hayo.
chanzo: zanzibarleo.

Comments