Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imejipanga kuboresha Wakala wa Ndege
za Serikali (TGFA) ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo
zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali
Hayo
yameelezwa na Naibu Waziri wa Uchukuzi na Mawasiliano wa Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Atashasta Nditiye wakati wa
ziara yake ya kikazi alipotembelea na kukagua utekelezaji wa majukumu ya
Wakala wa Ndege za Serikali ambayo inasimamia na kuendesha ndege ambazo
zinasafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali ambapo alizungumza na
Menejimenti na wafanyakazi na kuwaeleza kuwa Serikali imejipanga
kuboresha Wakala hiyo
Mhandisi
Nditiye alisema kuwa azma ya Serikali ya Awamo ya Tano inayosimamiwa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli
ni kuhakikisha kuwa Taasisi za Serikali zinafanya kazi zake kwa weledi
na uadilifu ili kufanikisha malengo ya Serikali ya kuwatumikia
wananchi.
“Serikali
inatambua umuhimu wa Wakala hii na ina imani kubwa nanyi katika
kuhakikisha kuwa mnafanya kazi zenu za kusafirisha viongozi kwa usalama
na kwa uhakika ili waweze kutimiza majukumu yao ya kuwatumikia wananchi
na tayari ina nia ya kuboresha taasisi hii”, amesema Mhandisi Nditiye.
Naye
Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa TGFA Bwana Tito Kasambala amemueleza
Mhandisi Nditiye kuwa taasisi yake ina ndege nne ambazo zinatumika
kusafirisha viongozi wa kitaifa wa Serikali katika kutimiza majukumu yao
ya kuwatumikia watanzania na tayari Serikali imetenga shilingi bilioni
11.4 kwenye bajeti ya mwaka wa fedha wa 2017/18 kwa ajili ya shughuli
mbali mbali za Wakala ikiwemo matengenezo ya ndege, mafunzo kwa wanahewa
na ukarabati wa karakana.
Mhandisi
Nditiye amewaeleza wajumbe wa Menejimenti na wafanyakazi wa Wakala hiyo
kuwa Serikali inatambua na kuthamini mchango wao na umuhimu wa
wahandisi wa ndege na marubani wa kupata nafasi ya kuendesha ndege na
kozi za mafunzo mbali mbali kuendana na taaluma zao ambapo tayari
makubaliano yamefanyika baina ya Wizara na Shirika la Ndege Tanzania
(ATCL) ya kuwapatia nafasi marubani wa ndege za Wakala wa Ndege za
Serikali nafasi ya kurusha ndege mara kwa mara ili kuendana na matakwa
ya taaluma zao.
Ameongeza
kuwa Serikali inashughulikia suala la miundo ya watumishi wa umma
ambapo Wakala wa Ndege za Serikali ni mojawapo ya taasisi ambayo muundo
wake unafanyiwa kazi ili kuweza kuzingatia taaluma, kada za watumishi na
maslahi yao.
“Natumaini
wote mnatambua na kuelewa kuwa kipindi cha hapo nyuma kidogo utumishi
wa umma uliingiwa na baadhi ya watu wachache ambao walikuwa wanafanya
ujanja ujanja na kuharibu utumishi wa umma ambapo Serikali ya Awamu ya
Tano chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais wetu,
imelifanyia kazi jambo hili na ameunda bodi maalumu ambayo inafanyia
kazi suala la muundo, kada na maslahi ya watumishi wa umma,” amesema
Mhandisi Nditiye.
Aidha,
wafanyakazi wa Wakala wa Ndege za Serikali wamemuomba Mhandisi Nditiye
kuwasilisha ombi lao kwa Serikali la kuwaongezea mishahara yao kuendana
na hali ya soko la ajira ya marubani ilivyo nchini kwa sasa.
Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini,
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
chanzo:Mpekuzi.
Comments