
Uongozi wa juu wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini umesema umepokea kwa mshituko taarifa ya msiba huo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Freeman Mbowe, Kimesera alifariki dunia usiku wa kuamkia juzi.
“Chadema tumepokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za msiba huu. Tumeondokewa na moja ya nguzo muhimu za ustawi wa chama chetu ambaye amekuwa katikati ya mapambano tangu aliposhiriki kuasisi chama hiki hadi umauti ulipomkuta akiwa mtendaji wa chama makao makuu,” Mbowe alisema katika taarifa hiyo.
“Kimesera maarufu kama VPK kama tulivyozoea kumuita, ametutoka katika kipindi ambacho mchango wake ungehitajika sana, hasa wakati huu ambapo taifa letu linapita katika mkwamo mkubwa wa kisiasa.
Atakumbukwa zaidi kwa namna alivyojitolea kwa hali na mali kupigania haki, demokrasia na maendeleo nchini na kipekee katika Jimbo la Kiteto mkoani Manyara.”
Katika taarifa yake hiyo, Mbowe alisema kwa sasa chama kupitia ofisi ya Katibu Mkuu kinashirikiana na familia ya marehemu kuhusu taratibu mbalimbali za msiba huo na ratiba ya mazishi yanayotarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam zitatolewa baadaye.
chanzo:Mpekuzi.
Comments