Mkuu
wa Mkoa wa Manyara, Alexander Mnyeti ametengua agizo la Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dk Hamisi Kigwangalla aliyewapa miezi tisa wananchi
wa Kijiji cha Kimotorok kuondoka katika maeneo wanayoishi wakidaiwa
kuvamia Hifadhi ya Tarangire wilayani Simanjiro.
Akizungumza
na wanakijiji hao juzi, Mnyeti alisema hakuna atakayekwenda kuwafukuza
na kama hilo lipo, yeye ndiye atawaambia wanafukuzwa au la, hivyo wawe
na amani.
Mnyeti alisema ofisi ya mkoa inajiandaa kutuma wataalamu kwenda kupima eneo hilo ili kutatua mgogoro.
Februari
25, Waziri Kigwangalla aliwapa wananchi wa kijiji hicho, vitongoji vya
Massas na Loon’benek miezi tisa wawe wamehama kwa kuwa wamevamia eneo la
Hifadhi ya Tarangire.
Baadaye
alitoa ufafanuzi akisema kabla ya kuondoka, Serikali itawalipa fidia na
watatafutiwa maeneo mengine ikiwa ni pamoja na kujengewa zahanati nje
ya hifadhi kutokana na iliyokuwapo kuwa ndani.
Dk
Kigwangalla alipotafutwa jana kuzungumzia kauli ya Mnyeti alisema,
“Sijapata taarifa rasmi kwa maandishi. Siwezi kufanyia kazi taarifa za
kwenye mitandao. Nitasubiri barua kama itakuja. Hata hivyo, sina hakika
kama mkuu wa mkoa anaweza kusema hivyo.”
Mkuu
wa mkoa Mnyeti alitoa kauli baada ya msafara wake kusimamishwa na
wananchi wa Kimotorok alipokuwa akienda kwenye mkutano wa kuwapokea
wanachama zaidi ya 3,000 wa CCM kutoka vyama vingine.
Wananchi
wa kijiji hicho walimuomba mkuu wa mkoa kuingilia kati suala hilo kwani
watu wa hifadhi wanataka kuwapora ardhi yao bila hata kuwashirikisha
katika jambo lolote wanalofanya, ikiwamo kuweka alama ndani ya ardhi ya
kijiji hicho ambacho kina hati miliki tangu mwaka 1970.
Akijibu
hoja za wananchi, Mnyeti aliomba apewe siku 10 awe amefanya utaratibu
wa kupeleka wataalamu kutoka Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya
Makazi ambao wako katikati ya wananchi na hifadhi hivyo hawatapendelea
upande wowote.
“Sasa
chagueni kamati ndogo au Serikali ya kijiji watakaokwenda na wataalamu
kukagua alama za mipaka. Watapitia mipaka yote kujua ramani maana
hifadhi nayo ina umuhimu wake, hivyo muwe tayari kukubaliana na majibu
yatakayosomwa na mtaalamu baada ya ukaguzi maana hata ofisi ya ardhi
mkoa haijui utekelezaji wa uwekaji alama hizo,” alisema Mnyeti.
Alisema,
“Lakini pia inawezekana mko sahihi maana tunajua hawa watu wa hifadhi
mara nyingi wao wanataka kusogeza tu eneo, kila siku wanataka eneo
liongezeke, leo anaweza akaja akaishia hapa kesho akija anaishia hapa,
sasa tunaleta mtu ambaye yuko katikati ya hifadhi na wananchi na atapima
kuleta ukweli.”
chanzo:Mpekuzi.
Comments