Mkuu wa Majeshi: Kuna Viashiria vinavyotishia Usalama wa Nchi, Hatua zinachukuliwa kudhibiti hali hiyo.
Mkuu
wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama (JWTZ), Jenerali Venance Mabeyo
amewataka Watanzania kujiepusha na vitendo vinavyoweza kutishia usalama
wa nchi na kuharibu tunu ya amani iliyopo.
Ameeleza kuwa hivi sasa vipo viashiria vinavyotishia usalama wa nchi, na kwamba hatua zinachukuliwa ili kudhibiti hali hiyo.
Jenerali
Mabeyo amewaomba Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais
John Magufuli dhidi ya wizi, ufisadi na matumizi mabaya ya ofisi za
umma, kwa kuwataja hadharani watu wanaojihusisha na vitendo hivyo.
Ametoa
kauli hiyo jana wakati akifunga Maadhimisho ya Tamasha la Mashujaa wa
Vita ya Majimaji katika Viwanja vya Makumbusho ya Mashujaa wa Vita ya
Majimaji mjini Songea.
Mabeyo
amesema vita dhidi ya wizi na ufisadi, iliyoanzishwa na Rais Magufuli,
si ya mtu mmoja, bali kila Mtanzania anapaswa kushiriki, kwani mali
zinazoibwa na baadhi ya Watanzania, zinapaswa kuwanufaisha watu wote.
Mabeyo
alisema badala ya kushughulika na uvunjifu wa amani, ipo haja ya
Watanzania kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya
Tano, ambayo imedhamiria kuwatumikia wananchi kwa kuboresha huduma za
kijamii ili kutoa fursa kwa wananchi kutumia muda wao kufanya kazi za
kujiletea maendeleo.
Ametaja
baadhi ya mambo yanayotishia usalama wa nchi kuwa ni matumizi mabaya ya
utandawazi ambayo mbali na ya kuharibu utamaduni wa nchi, baadhi ya
watu wanaitumia vibaya kwa kuhamasisha wananchi kufanya na kushiriki
katika matukio ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani na utulivu uliopo
nchini kwa muda mrefu.
Jenerali
Mabeyo alitaka shule za msingi, sekondari na vyuo nchini, kufundisha
wanafunzi umuhimu wa kulinda, kutunza amani na wananchi kuishi kwa
kupendana, badala ya kutumia muda wao kutafuta sababu za kutengana,
jambo ambalo halina tija kwa taifa.
Wakati
huo huo, Jenerali Mabeyo aliitaka Wizara ya Maliasili na Utalii
kuboresha Makumbusho ya Mashujaa wa Vita ya Majimaji ili yatumike kwa
ajili ya utalii na kuliingizia taifa fedha nyingi.
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Chiristina Mndeme alisema Serikali ya Mkoa wa
Ruvuma, itaongeza nguvu katika kulinda mipaka yake ili wananchi wa mkoa
huo waweze kuendelea na kazi za uzalishaji mali.
chanzo:Mpekuzi.
Comments