Mkizubaa tu, tumewaumiza.

NYOTA wa Yanga jana walianza tizi kujiandaa na mechi yao ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Township Rollers ya Botswana, huku wakionekana kuwa na mzuka kinoma hasa baada ya kusikia Simba ilikomaliwa na Stand United juzi Ijumaa.
Sare ya mabao 3-3 iliyopata Simba imewafanya nyota hao wa Yanga kupata furaha ya ajabu na kuwatamkia watani wao kuwa; ‘Walahi wakizubaa tu, tumewaumiza, kwani tunataka tena ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu.’
Yanga ipo nafasi ya pili nyuma ya Simba kwa tofauti na alama sita, Simba ikiwa na 46 baada ya mechi 20 wakati Jangwani wana 40 na mechi mmoja mkononi kwani wamecheza michezo 19 tu.
Yanga wanaamini sare hiyo imewapa upenyo wa kuwanyoosha watani wao na beki Juma Abdul alisema kitendo cha Simba kugawana pointi na Stand kimewarudisha rasmi katika mbio za ubingwa.
Abdul alisema uongozi wao ulitumia akili kubwa kuomba mchezo wao na Mtibwa kusogezwa mbele kwani ungeweza kuwatibulia hesabu zao kutokana na uchovu mkubwa wa mechi walionao kwa sasa.
“Uongozi ulitumia akili sana, unajua kama tungecheza ile mechi ya Mtibwa Sugar haya ya Simba yangeweza kututokea lakini wenzetu waliona kama hesabu zao ziko sawa na sasa wanajuta. Ligi ni ngumu, pia mashindano ya Kimataifa pia ni magumu ni lazima mjue kujipanga,” alisema Abdul.
“Hii sare ya Simba tuliposikia wakati tunatoka mazoezini, hatukuamini na sasa kuna kitu kimeongezeka kwetu. Tukimaliza mechi hii ya Kimataifa na kurudi katika ligi hakuna atakayetoka salama, Simba imeturudishia pumzi halisi ya kuchukua ubingwa,” alisisitiza Abdul ambaye ni mchezaji bora wa Ligi Kuu Bara 2016.
Naye Hassan Kessy alisema kilichowaponza Simba ni tabia ya timu yao kutegemea nguvu ya watu wachache kitu ambacho kwao Yanga makocha wao walishakiondoa.
Kessy alisema Simba ilionyesha wazi kuhitaji huduma ya washambuliaji wao wawili nahodha John Bocco na Emmanuel Okwi.
“Hii sare kwetu imetuongezea nguvu, kila mmoja wetu sasa akili yake ni kuongeza nguvu, ushindani wa nafasi uliopo katika kikosi chetu ndiyo huo tutakaoutumia kuongeza kasi yetu ya kushinda ili kupunguza zaidi tofauti ya pointi, bado ubingwa uko ndani ya mikono yetu kwa sasa,” alisema.
NGOMA MDOGO     MDOGO
Wakati huo huo, habari njema kwa Yanga ni kwamba staa wao, Donald Ngoma ameanza mazoezi taratibu ndani ya kikosi hicho na jana Jumamosi alikimbia kwa dakika 30 na kutuliza mzuka kwanza.
Ngoma ambaye alikuwa nje kwa muda mrefu ameanza mazoezi hayo hivi karibuni na jana alishuhudiwa na Mwanaspoti akijifua pembeni ya uwanja wakati wenzake wakiwa katika mazoezi makali.
Katika mazoezi hayo yaliyofanyika jana asubuhi katika viwanja vya Gymkhana, Ngoma alitumia dakika hizo kisha kufanya mazoezi mengine mepesi na kupumzika.
Kurejea kwa Ngoma ambaye amekuwa nje ya uwanja tangu mwishoni mwa Septemba ni faraja kwa Yanga, ambayo inakimbizana na mashindano matatu makubwa kwa sasa ambayo ni Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Bara na kombe la FA.
Daktari wa muda wa Yanga Richard Yomba alisema bado mshambuliaji huyo aliyeifungia timu hiyo mabao 41 kwenye mashindano hayo tangu alipojiunga nayo Julai 2015, anaendelea kufanya mazoezi taratibu ikiwa ni programu maalumu aliyopewa baada ya kupona.
“Ni programu aliyopewa baada ya kuanza kupona na ataifanya kwa muda maalumu kabla ya kuingia katika mazoezi mengine kulingana na hali itakavyoendelea,” alisema Yomba.

Comments