Hali hiyo ilitokana na umati mkubwa wa wafuasi wa Chadema wakiongozwa na mawaziri wakuu wa zamani, Edward Lowassa na Frederick Sumaye waliofika mahakamani hapo kusikiliza kesi inayowakabili viongozi sita wakuu wa chama hicho, akiwamo mwenyekiti, Freeman Mbowe ambao hawakufikishwa Kisutu kutoka Gereza la Segerea, ikielezwa kuwa gari lilipopaswa kuwafikisha hapo liliharibika.
Mbali na Mbowe, viongozi wengine wanaokabiliwa na mashtaka hayo ni katibu mkuu, Dk Vincent Mashinji; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; manaibu katibu wakuu, John Mnyika (Bara) na Salum Mwalimu (Zanzibar); na mweka hazina wa Baraza la Wanawake la chama hicho (Bawacha), Esther Matiko.
Licha ya kutokuwapo, shauri lao la dhamana lilisikilizwa na hakimu mkazi mkuu wa mahakama hiyo, Wilbard Mashauri kueleza kuwa ipo wazi jambo ambalo liliibua malumbano ya kisheria kati ya upande wa Serikali na utetezi na hakimu huyo kuamuru washtakiwa hao wafikishwe mahakamani hapo Jumanne ijayo ikimaanisha kwamba watendelea kukaa mahabusu mpaka Sikukuu za Pasaka zitakapomalizika.
Hakimu Mashauri alisema siku hiyo washtakiwa watasaini hati ya Sh20 milioni na kuachiwa kwa dhamana.
Wakati hayo yakiendelea mahakamani, baadhi ya wabunge na madiwani wa chama hicho waliandamana kwenda ofisi za Umoja wa Ulaya (EU) kuwasilisha kile walichoeleza kuwa ni masuala mbalimbali yaliyowakumba viongozi hao, ikiwa ni pamoja na vikwazo vya kupewa dhamana.
Viongozi hao wa Chadema wanakabiliwa na jumla ya makosa manane, likiwamo la kuhamasisha uasi, chuki na maandamano yaliyosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilini.
Kati ya makosa hayo, mawili yanawakabili washtakiwa wote sita ambayo ni kufanya mkusanyiko au maandamano yasiyo halali Februari 16 wakidaiwa kufanya hivyo wakiwa Barabara ya Kawawa, Kinondoni Mkwajuni.
Katika shtaka la pili, wanadaiwa wakiwa na watu wengine 12 ambao hawajafikishwa mahakamani, waligoma kutii amri ya kusambaratika na kuvunja mkusanyiko huo uliosababisha kifo cha Akwilina huku maofisa wa polisi wakipata majeraha.
Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni anadaiwa kuhamasisha chuki kwa wanajamii isivyo halali na ushawishi wa utendekaji wa kosa la jinai. Mchungaji Msigwa anashtakiwa akidaiwa kushawishi raia kutenda kosa la jinai.
Ilivyokuwa
Washtakiwa hao walipandishwa kizimbani kwa mara ya kwanza Februari 27 na kesi yao kuahirishwa hadi jana kwa ajili ya kusomewa uamuzi dhamana.
Jana, katika kesi hiyo ambayo ilianza saa 8:17 mchana hadi saa 10:40 jioni, hakimu Mashauri aliutaka upande wa Jamhuri kuwaleta Mbowe na wenzake ili kukamilisha masharti ya dhamana waliyopewa ambayo yalikuwa kila mmoja kuwa na wadhamini wawili wenye barua za uongozi wa mtaa au kijiji na nakala za vitambulisho vyao.
Pia, walitakiwa kuripoti Kituo Kikuu cha Polisi kila Alhamisi. Alitoa nafasi kwa asiyeridhika na uamuzi huo kukata rufaa.
Baada ya Hakimu Mashauri kutoa uamuzi, wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi aliwasilisha taarifa ya kukata rufaa chini kifungu cha 379 (1)(a) cha sheria ya makosa ya jinai na sheria ya huduma ya mashtaka ya Taifa.
Baada ya kueleza hayo wakili wa upande wa utetezi, Peter Kibatala alisema kwa wakati huo Mahakama haikuwa na mamlaka ya kurekodi taarifa ya rufaa iliyotolewa kwa sababu masharti ya dhamana hayajakamilika.
Akitoa ufafanuzi kuhusu rufaa hiyo, wakili Nchimbi alidai kuwa taarifa ya kukata rufaa wameiwasilisha kwa mujibu wa sheria baada ya Mahakama kutoa masharti ya dhamana na kueleza haki ya kukata rufaa ipo wazi.
Alidai kuwa hilo ni suala la kisheria na kwamba taarifa ya kukata rufaa ilishafailiwa mahakamani na ikapokewa na kwamba haina mamlaka ya kurudi nyuma kufuta yale ambayo imekwisha yarekodi.
Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alisisitiza kuwa taarifa hiyo ya kukata rufaa imetolewa kwa wakati sahihi kwa sababu Mahakama ilikwishatoa amri ya kuwapa dhamana washtakiwa na masharti ya dhamana.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri alisema taarifa hiyo ya rufaa haiwezi kukubalika kwa sababu imewasilishwa katika muda usio sahihi.
Hivyo, aliamuru Mbowe na wenzake watano wafikishwe Kisutu Jumanne ijayo kusaini hati ya dhamana ya Sh 20 milioni na wakishaachiwa, ndipo suala la kukata rufaa lifanyike.
Awali, Wakili Nchimbi, aliiambia Mahakama kuwa upelelezi wa kesi hiyo umekamilika, lakini washtakiwa hawakuwapo na kwamba alifanya mawasiliano na inspekta wa Magereza aliyemtaja kwa jina moja la Shabani ambaye alisema ndiye msimamizi wa mahabusu ambaye aliwasiliana na uongozi wa Segerea na kuambiwa kuwa mahabusu kutoka gereza hilo hawakufika kwa tatizo ambalo atalielezea.
Inspekta Shabani, aliieleza Mahakama kuwa jana asubuhi alifanya mawasiliano na mkuu wa gereza lakini hakumpata. Alifanikiwa kumpata msaidizi wake aliyeeleza kuwa wakati akitoka gerezani, gari liliharibika.
Alidai kuwa aliwasiliana nao mchana wakamueleza kuwa gari hilo bado halijatengemaa na imeshindikana kuwapeleka mahakamani.
Baada ya kusikiliza hoja hizo, Hakimu Mashauri alisema kwa sababu ambazo zimetolewa atatoa uamuzi hata kama washtakiwa hawapo mahakamani.
Hali ilivyokuwa
Kutokana na ulinzi kuimarishwa kuanzia saa 12 asubuhi, wafuasi wengi wa Chadema walijazana nje ya Mahakama hali iliyowafanya polisi kuongeza ulinzi katika maeneo mbalimbali.
Baadhi ya watu waliofika mahakamani hapo na kushindwa kujieleza vyema kilichokuwa kimewapeleka hawakuruhusiwa kuingia.
Lowassa ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema alifika mahakamani hapo saa 2:21 asubuhi na kufuatiwa na Sumaye.
Ilipofika saa 4:54 asubuhi viongozi hao waliondoka na kwenda katika mazishi ya muasisi wa chama hicho, Victor Kimesera aliyefariki dunia Machi 24.
Wakati wote huo, wafuasi wa Chadema waliokuwa wamezuiwa kuingia walikuwa nje ya uzio wakiimba nyimbo mbalimbali na kutaja majina ya viongozi walioshtakiwa.
Lowassa alirejea mahakamani hapo Saa 7:49 mchana.
Kilichojiri EU
Wakizungumza baada ya kutoka ubalozi wa EU, Meya wa Ubungo, Boniface Jacob alisema miongoni mwa mambo waliyowaeleza wawakilishi hao wa Jumuiya ya Ulaya ni; ukandamizaji wa demokrasia na utawala bora, kitendo cha viongozi wao kuendelea kusota gerezani, matukio ya mauaji na utesaji kwa viongozi na wanachama Chadema pamoja na nguvu inayotumiwa na Jeshi la Polisi.
Jacob ambaye pia ni diwani wa Ubungo alisema suala mengine ni kukwama kwa mchakato wa Katiba Mpya na uhuru wa Mahakama.
“Tumewaomba kusitisha misaada kutoka kwa wahisani na kutokuchangia katika bajeti ya Serikali kutokana na matukio haya.”
Baadhi ya wabunge zaidi ya 20 waliofika kwenye ofisi hizo ni; Godbless Lema (Arusha Mjini), Cecil Mwambe (Ndanda), Peter Lijualikali (Kilombero), Joseph Haule ‘Profesa Jay’ (Mikumi), Jesca Kishoa, Cecilia Paresso, Anatropia Lwehikila Theonest, Suzan Mwakagenda (wote wa Viti Maalumu).
chanzo:Mwananchi.
Comments