Mkurugenzi
wa Kampuni inayoandaa mashindano ya Miss Tanzania ya Lino International
Agency LTD Hashim Lundenga ametangaza rasmi kuacha shughuli za
kuendesha mashindano hayo kuanzia Februari 13 mwaka huu.
Hivyo
kuanzia sasa mashindano ya Miss Tanzania nchini yataendeshwa na The
Look Company Limited, chini ya Mkurugenzi Basilla Mwanukuzi aliyewahi
kuwa Miss Tanzania mwaka 1998.
Akizungumza
jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa kampuni hiyo, Hashim Lundenga
amesema uamuzi huo umetokana na malengo yao ya kutaka mashindino hayo
kusimamiwa na damu changa kwa lengo la kuleta chachu katika tasnia ya
urembo nchini.
“Tumefikia
uamuzi huu baada ya kuona kampuni yetu tayari imejijengea sifa na
heshima nchini.Hata hivyo tunaamini The Look Company Limited chini ya
Mkurugenzi Mwanukuzi watasimamia taratibu, kanuni, sheria na miiko ya
uongozi na hatimaye kumpeleka mrembo katika mashindano ya dunia kama
ilivyo kawaida,”amesema.
Amewataka waandaaji wapya wa mashindano ya urembo wasisite kuomba ushauri au mawazo ya kujenga kutoka kwao pale watakapohitaji.
Lundenga
ambaye ni maarufu kama Uncle Hashim amewashukuru Baraza za sanaa la
Taifa (BASATA), na Wizara ya Habari, Utamaduni,Sanaa na Michezo kwa
ushirikiano mkubwa kwa muda wote tangu kuanza kwa mashindano hayo mwaka
1994.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa Kampuni ya Look Limited, Mwanukuzi amesema
wamejiwekea mikakati kuendeleza fani ya ulimbwende pale ambapo kampuni
ya Lino imeishia. Amesema kuwa pale penye changamoto katika kuandaa
masuala ya warembo watakuwa karibu na Kampuni ya Lino pamoja na BASATA
ili kufanikisha na kuleta tija katika Taifa.
chanzo:Mpekuzi.
Comments