Leo ni Jumanne tarehe 6 Machi, 2018.

Jumanne tarehe 6 Machi, 2018Leo ni Jumanne tarehe 17 Jamadithani 1439 Hijria sawa na 6 machi 2018.

Siku kama ya leo miaka 543 iliyopita, alizaliwa mjini Caprese Michelangelo, mchoraji na mhunzi wa masanamu wa Italia. 
Licha ya upinzani mkubwa wa baba yake juu ya fani hiyo ya uhunzi na uchoraji, Michelangelo alijiendeleza katika fani hiyo na kupata umahiri mkubwa. 
Uhodari wake ulionekana miaka michache baadaye, ambapo alifanikiwa kuchonga masanamu mengi ya kuvutia. 
Michelangelo, alitokea kuwa mhunzi hodari wa karne ya 16 Miladia. Mwaka 1505, wakazi wa mji wa Roma walimwalika Michelangelo, ili aende kuwachongea sanamu la papa kwenye kaburi lake.
 Baadaye papa wa wakati huo, alimtaka mtaalamu huyo kupamba paa la kanisa la Sistine, kazi iliyoanza hapo mwaka 1508 na kumalizika mwaka 1512 Miladia. Mbali na hayo, Michelangelo alichonga sanamu kubwa la Nabii Issa (as), ambalo lipo mjini Roma hadi leo.
Siku kama ya leo miaka 466 iliyopita yaani tarehe 6 Machi 1552, vilimalizika vita vikubwa vya pili kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ujerumani, kwa kushindwa Waprotestanti. Vita hivyo vilipiganwa nchini Austria. Sababu ya vita hivyo zilikuwa za kimadhehebu na vilianza baada ya Martin Luther kuanzisha madhehebu ya Kiprotestanti katika dini ya Kikristo.
Tarehe 6 Machi miaka 61 iliyopita, nchi ya Ghana ilifanikiwa kupata uhuru chini ya uongozi wa Dakta Kwame Nkurumah. Ghana ilitumbukia katika makucha ya mkoloni wa Kireno kuanzia karne ya 15. Baada ya Wareno, Waingereza waliidhibiti na kuikoloni nchi hiyo iliyokuwa mashuhuri kwa jina la "Pwani ya Dhahabu" kutokana na utajiri wake mkubwa wa madini hayo.
Miaka 118 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia mvumbuzi wa Kijerumani Gottlieb Daimler akiwa na umri wa miaka 64. 
Daimler alizaliwa mwaka 1834 na kazi yake ya mwanzo ilikuwa utengenezaji bunduki. 
Tangu akiwa kijana mvumbuzi huyo alivutiwa sana na kazi za viwandani na alifanya utafiti mkubwa katika uwanja huo hadi alipofanikiwa kutengeneza pikipiki. Gottlieb Daimler pia alikuwa miongoni mwa watu walioweka misingi ya utengenezaji wa magari madogo na hata mabasi.
Siku kama ya leo miaka 119 iliyopita yaani tarehe 17 Jamaduth Thani mwaka 1320 Hijiria, alifariki dunia msomi wa Kiislamu Hajj Mirza Husain Nuri Tabrasi. Msomi huyu mkubwa alifikia daraja ya juu katika ibada, ucha-Mungu na ukamilifu wa nafsi. 
Hajj Mirza Hussein hakuwa mbali na uandishi wa vitabu. Vitabu vyake vingi vilihusu elimu za hadithi, tafsiri na ufafanuzi kuhusiana na maisha ya wasomi wa Kiislamu na masuala mengine muhimu. Aidha Nuri Tabrasi alilipa umuhimu mkubwa suala la kueneza athari za Ahlul Bait wa Mtume (saw). 
Hadi sasa zipo athari kadhaa kutoka ustadhi Hajj Mirza Hussein Nuri Tabrasi, ambapo miongoni mwa athari zake mashuhuri ni pamoja na kitabu kiitwacho "Mustadrakul Wasaail" ambacho kimeshamili habari za hadithi na ufafanuzi wa hali za maulama wa Kiislamu.
 Hii nikwahisani ya parstoday.

Comments