Kushindwa maadui mbele ya mhimili wa muqawama kwa mtazamo wa Kiongozi Muadhamu.

Kushindwa maadui mbele ya mhimili wa muqawama kwa mtazamo wa Kiongozi MuadhamuKiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa, Syria leo hii iko katika mstari wa mbele wa muqawama hivyo basi ni jukumu letu kuunga mkono kusimama kidete nchi hiyo na kwamba, Rais wa Syria Bashar al Assad amedhihirika katika sura moja ya mwana muqawama mkubwa na kwamba yupo imara na hakuna shaka yoyote kuhusu Rais Assad; na jambo hilo ni muhimu sana kwa nchi yoyote ile.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei alisema hayo Alkhamisi ya jana alipoonana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Wakfu wa Syria Dk. Mohammad Abdul-Sattar al-Sayyed na ujumbe wa maulamaa aliofuatana nao hapa Tehran na kubainisha kwamba, madhila ya baadhi ya mataifa chimbuko lake ni udhalili wa viongozi. 
Kiongozi Muadhamu amesema bayana kwamba, adui hawezi kufanya jeuri yoyote mbele ya taifa lenye izza na heshima ambalo viongozi wake wanahisi kuwa na izza na heshima na wanaona fahari na Uislamu na utambulisho wao.
Maadui wa mhimili wa muqawama  wakitumia kisingizio cha kuwaunga mkono wananchi wa Syria, kuanzia Machi 2011 walianzisha njama zao dhidi ya Syria ikiwa ni mhimili wa muqawama dhidi ya utawala dhalimu wa Israel. 
Njama hizo za maadui zilikwenda sambamba na kuibuka wimbi la mwamko wa Kiislamu katika eneo la magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) na kaskazini mwa Afrika.
Kwa hakika Syria ilikuwa ngome imara na isiyopenyeka mbele ya siasa za tamaa na za kupenda makuu za utawala ghasibu wa Israel na kikwazo kwa mipango michafu ya Marekani na washirika wake kwa ajili ya kuanzisha Mashariki ya Kati Kubwa. 
Ni kwa mintarafu hiyo, ndio maana Syria ikaanza kuandamwa na njama mtawalia na vita vya niaba vilivyofanywa dhidi yake kwa kuwakodisha magaidi.
Kupelekwa nchini Syria magaidi waliokusanywa kutoka katika maeneo mbalimbali duniani na kupatiwa misaada ya kifedha na silaha, kulikuwa na lengo moja muhimu tu, nalo ni kuuangusha utawala thabiti na usio kibaraka wa Rais Bashar al-Assad na hivyo kuziandalia mazingira mazuri njama za maadui dhidi ya mhimili wa muqawama. 
Hata hivyyo kusimama imara Rais Assad na wananchi wa Syria mbele ya magaidi wa kukodishwa katika vita vya niaba kulisambaratisha ndoto za madola makubwa kwani mipango yao iliota mbawa.
Hii leo nchi ya Syria kutokana na kusimama kwake kidete inaungwa mkono kila upande na Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwani nchi hiyo imesimama katika mstari wa mbele wa kupambana na maadui wa Uislamu. 
Uungaji mkono wa kiushauri wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran kwa Syria sambamba na kusimama kidete kiongozi wake na wananchi wa nchi hiyo kumezuia kabisa kutekelezwa njama za maadui kwa maslahi ya utawala haramu wa Israel. 
Kivitendo hali hiyo imesambaratisha kabisa njama za kuigawa Syria hatua ambayo ingekuwa utangulizi wa kutekelezwa mpango wa kuanzishwa Mashariki ya Kati Kubwa.
Kutofua dafu maadui wa Ulimwengu wa Kiislamu mbele ya wananchi wana mapambano kumethibitisha kwamba, endapo taifa fulani litakuwa na kiongozi imara na asiyekubali kuburuzwa, mwenye moyo wa mapambano na kutaka izza na heshima, basi ataibuka na ushindi katika uwanja wa vita na kumbwaga adui. 
Hii leo Kiongozi wa Syria Bashar al-Assad na wananchi wake ni nembo ya mafanikio haya. 
Kusimama kidete kwa ajili ya kutetea utambulisho wa taifa la Syria baada ya kupita miaka saba tangu nchi hiyo itwishwe vita kumethibitisha kwamba, adui hawezi kufikia malengo yake mbele ya taifa kama hili. 
Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni mfano mwingine hai, mapinduzi ambayo yamekataa katakata kusalimu amri mbele ya uafriti na vitisho vya maadui. 
Kwa hakika majimui ya mhimili wa muqawama ambao leo una nafasi muhimu huko Syria, imegeuza mahesabu ya magharibi mwa Asia (Mashariki ya Kati) na kuyafanya kuwa kwa maslahi ya wananchi. 
Kufikia tamati Khilafa ya kujipachika ya kundi la kigaidi la Daesh huko Iraq na Syria ilikuwa kilele cha nafasi muhimu, athirifu na yenye utendaji mzuri ya wapiganaji shupavu wa muqawama huko Lebanon, Syria na Iraq.
Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Ali Akbar Velayati, mshauri wa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika masuala ya kimataifa akasisitiza kwamba, mhimili wa muqawama umeziokoa Baghdad, Damascus na Beirut na shari ya kundi la kigaidi la Daesh.
chanzo:parstoday.

Comments