MZUNGUKO wa 18 wa Ligi Kuu Zanzibar kanda ya Unguja umemaliza jana huku timu ya Polisi ikiondoka na ushindi, baada ya kuzidi kuikandamiza chini timu ya Kipanga kwa kuifunga mabao 3-1.
Mchezo huo ulipigwa katika dimba la Amaan majira ya saa 10:15 jioni
ambao ulikuwa mkali na kupendeza kwa muda wote, ambapo licha ya kufungwa
Kipanga ilicheza kwa juhudi zote lakini haikufanikiwa kutoka na
ushindi.
Polisi ilianza kuonesha dalili za ushindi mwanzoni tu mwa kipindi cha
kwanza baada ya kupata bao la kuongoza, lililokwamishwa wavuni na
mchezaji Suleiman Nuhu dakika ya 15, bao ambalo liliweza kudumu hadi
kipindi cha kwanza kinamalizika.
Kipindi cha pili kila timu ilirudi uwanjani na nguvu mpya zaidi
Kipanga ikicheza kutafuta bao la kusawazisha, lakini Polisi wakitafuta
bao jingine, na mbinu za Kipanga zilifanikiwa kupata bao la kusawazisha
dakika ya 50 lililofungwa na Ramadhani Ajal.
Hata hivyo bao hilo halikudumu sana kwani Kipanga wakiendelea
kusherehekea walijikuta wakipachikwa bao la pili, dakika ya 53
lililofungwa na Suleiman Mwalimu.
Baada ya mabao hayo kila timu ilizidisha mashambulizi langoni mwa
mwenzake kila mmoja akitafuta bao, lakini bahati ikaenda kwa Polisi
waliofanikiwa kuandika bao la tatu lililofungwa tena na mchezaji
Suleiman Mwalimu dakika ya 70.
Kwa upande wa kanda ya Pemba timu ya Kizimbani imejiweka katika
mazingira magumu baada ya kuingia katika mstari wa timu sita
zitakazoteremka daraja msimu huu, baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-2
kutoka kwa timu ya FSC.
Mchezo huo uliopigwa katika uwanja wa Gombani, huku ukishuhudiwa na mashabiki wachache.
Comments