
Wakati Papii Kocha akisema alikuwa akijishughulisha na ushonaji wa
mazulia, Nguza amesema alichaguliwa kuwa mnyampala, akiwa na jukumu la
kusimamia wafungwa katika masuala mbalimbali.
Babu Seya, ambaye ni mtunzi wa kibao maarufu cha “Seya”,
na mwanae Papii Kocha ambaye wameshirikiana katika wimbo huo, ni
miongoni mwa wafungwa 8,157 waliosamehewa na Rais John Magufuli siku ya
Uhuru wa Tanganyika.
Walikuwa kati ya wafungwa 61 waliokuwa na adhabu za vifungo vya
maisha na kunyongwa ambazo si rahisi kupata msamaha wa kawaida wa mkuu
wa nchi unaotolewa siku ya sherehe hizo.
Wakihojiwa leo Ijumaa Machi 9, 2018 katika kipindi cha Leo Tena
kinachorushwa na Redio Clouds, Papii Kocha amesema wakati akiwa gerezani
alikuwa akifanya shughuli za ushonaji wa mazulia pamoja na vikapu.
“Nilikuwa sijui kabla ya kwenda gerezani lakini tulijifunza na kwa sasa naweza vizuri,” amesema.
Amesema mbali na ushonaji, pamoja na baba yake walikuwa wakifanya mazoezi ya muziki mara tatu kwa wiki.
Kwa upande wake Nguza amesema alivyokuwa gerezani alikuwa nyampala
mkuu wa gereza baada ya kuteuliwa na uongozi wa Jeshi la Magereza.
“Ni busara tu zilinifanya nikateuliwa. Kazi ilikuwa ngumu na isitoshe unaowaongoza ni wahalifu lakini busara tu ilitumika,” amesema.
chanzo: zanzibar24.
Comments