Miaka 24 iliyopita katika siku kama ya leo alifariki dunia Ayatullah Muhammad Ali Araki, mmoja wa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 103.
Mwanzuoni huyo wa Kiislamu alizaliwa katika mji wa Arak katikati mwa Iran na kujifunza elimu ya dini kwa maulamaa wakubwa hususan Ayatullahil Udhma Hairi.
Ayatullah Muhammad Ali Araki alifundisha katika chuo kikuu cha kidini cha Qum kwa kipindi cha miaka 35 na kulea wanazuoni na wasomi hodari.
Mwanazoni huyo mkubwa amezikwa katika Haram tukufu ya Maasuma (as) katika mji mtakatifu wa Qum.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel lilianzisha mashambulizi na uvamizi dhidi ya ardhi ya Lebanon kwa kisingizio cha kukabiliana na operesheni iliyofanywa na wanamapambano wa Kipalestina pambizoni mwa Tel Aviv.
Katika mashambulio hayo jeshi la Israel liliua raia wengi wasio na hatia wa Lebanon na Palestina na kukalia kwa mabavu sehemu ya ardhi ya Lebanon.
Hata hivyo utawala huo ghasibu uliondoka kwa fedheha katika maeneo ya kusini mwa Lebanon mwaka 2000, baada ya kupata kipigo kikali kutoka kwa wanamapambano wa Hizbullah na kuondoka kwenye eneo hilo.
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita sawa na tarehe 23 Esfand 1340 Hijria Shamsia, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Abul Qassim Kashani, mwanachuoni na shakhsia maarufu wa kisiasa katika historia ya Iran.
Ayatullah Kashani alifanikiwa kupata daraja la ijtihadi akiwa bado barobaro huko Najaf nchini Iraq lakini baadaye alifukuzwa nchini humo kutokana na misimamo yake ya kupinga ukoloni wa Uingereza.
Aliporejea nchini Iran, Ayatullah Kashani aliendelea na misimamo yake ya kupambana na ukoloni wa Uingereza na kufungwa jela mara kadhaa.
Baada ya kutoka jela wananchi wa Tehran walimchagua kuwa mwakilishi katika bunge la Taifa.
Miaka 64 iliyopita yaani mnamo mwaka 1954 tarehe 14 mwezi Machi vilianza vita vya kihistoria na vikubwa vilivyojulikana kwa jina la vita vya" Dien Bien Phu" ambavyo viliainisha mustakbali wa wanajeshi wa kikoloni wa Ufaransa huko Indochina.
Katika vita hivyo wapiganaji wa harakati ya wanamapinduzi ya Viet Minh waliokuwa wakipigania ukombozi wa Vietnam walipambana na jeshi la wakoloni wa Kifaransa waliokuwa katika ngome ngumu kudhibitiwa ya Dien Bien Phu.
Hatimaye tarehe 7 Mei mwaka huo huo vita hivyo vilifikia tamati kwa kusalimu amri kamanda wa majeshi ya Ufaransa aliyekuwa katika ngome ya Dien Bien Phu.
Vita hivyo viliwafungisha virago wakoloni wa Ufaransa nchini Vietnam.
Siku kama ya leo miaka 139 iliyopita alizaliwa Albert Einstein msomi mashuhuri wa fizikia na hisabati nchini Ujerumani.
Mnamo mwaka 1921 msomi huyo alifanikiwa kupewa tuzo ya Nobel katika taaluma ya fizikia baada ya kufanya juhudi kubwa za kiutafiti.
Utafiti na nadharia za Einstein katika uwanja wa nyuklia ulikuwa na athari kubwa duniani.
Hata hivyo Einshtein alisikitika sana baada ya kugundua kwamba, uchunguzi na utafiti wake katika uwanja wa atomu umetumiwa na baadhi ya nchi kwa ajili ya kutengeneza silaha hatari za nyuklia.
Albert Einstein alifariki dunia 1955.
Hii nikwahisani ya parstoday.
Comments