Kwa mujibu wa dikrii ya hivi karibuni ya Haider al-Abadi, Waziri Mkuu wa Iraq, wapiganaji wa Hashdu sh-Sha'abi watatakiwa kupewa mishahara sawa na wenzao jeshini kama ambavyo pia watajumuishwa katika sheria zote zinazohusiana na utumishi jeshini.
Akizungumza na gazeti la Asharq Al-Awsat, Naim al-Aboudi, Msemaji wa Harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq amesema kuwa uamuzi huo wa waziri mkuu wa Iraq kuihusu Hashdu sh-Sha'abi ina maana ya kulinganisha haki za wanamapambano wa harakati hiyo na jeshi la Iraq ingawa hiyo haimaanishi kuiunganisha harakati hiyo na idara ya usalama ya nchi hiyo.
Kufuatia amri hiyo ya Haider al-Abadi baadhi ya vyombo vya habari vimeanzisha propaganda kwamba hatua hiyo ni sawa na kuiunganisha harakati ya Hashdu sh-Sha'abi ndani ya idara ya usalama iliyo chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Ulinzi ya Iraq.
Al-Aboudi ameongeza kwamba, hatari ya kundi la ukufurishaji na kigaidi la Daesh (ISIS) bado ipo na kwamba matukio yaliyojiri hivi karibuni katika maeneo ya Mosul na Samarra yanathibitisha suala hilo.
Kadhalika amesisitiza kuwa, matukio hayo ya uvunjifu wa amani yamebainisha umuhimu na udharura wa kuendelea kuwepo wapiganaji wa Hashdu sh-Sha'abi katika maeneo tofauti ya Iraq kwa ajili ya kudhamini usalama.
Naye kwa upande wake Sheikh Qais Khazali, Katibu Mkuu wa harakati ya Asa'ib Ahl al-Haq amepongeza hatua ya Waziri Mkuu wa Iraq ya kusikiliza matakwa ya harakati hiyo ya wananchi ya kulinganisha haki za wapiganaji wa Hashdu sh-Sha'abi na jeshi la taifa.
chanzo:parstoday.
Comments