Inaelezwa kuwa, hali mbaya zaidi ya chakula ilishuhudiwa mwaka 2017 kaskazini mwa nchi ya Nigeria, Somalia, Yemen na Sudan Kusini ambako zaidi ya watu milioni 32 hawakuwa na chakula na walihitaji msaada wa haraka.
“Vita na majanga yanayohusiana na mabadiliko ya tabianchi vilileta madhara makubwa na kusababisha hali ya njaa kuongezeka baada ya miaka kadhaa ya hali hiyo kudhibitiwa.” imeongeza ripoti hiyo ya Umoja wa Mataifa na Umoja wa Ulaya.
Taarifa zaidi zinasema kuwa, kwa sasa maeneo mengi hayafikiki kuanzia barani Afrika, Mashariki ya Kati na sehemu za Asia Kusini ambako vita na hali tete ya usalama imesababisha kutokuwepo na usalama wa chakula.
Hata hivyo ukame uliokithiri kwenye nchi za pembe ya Afrika, mafuriko barani Asia na vimbunga kwenye nchi za America na visiwa vya Caribbean vyote hivi vilichangia kuenea kwa baa la njaa.
Ripoti hiyo imesema kuwa, mizozo na usalama mdogo huenda vikasalia kuwa changamoto kwa usalama wa chakula katika mwaka huu wa 2018 na kuathiri nchi za Afghanistan, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kaskazini mwa Nigeria, eneo la ukanda wa Ziwa Chad, Sudan Kusini, Yemen pamoja na Libya na eneo la kati la Sahel kwenye nchi za Mali na Niger.
Comments