Zarif: Kila mtu katika UNSC ameshuhudia usanii mchafu wa kuwaunga mkono walioanzisha uvamizi dhidi ya Yemen.

Zarif: Kila mtu katika UNSC ameshuhudia usanii mchafu wa kuwaunga mkono walioanzisha uvamizi dhidi ya YemenWaziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuhusu rasimu ya azimio "dhidi ya Iran" iliyowasilishwa na Uingereza katika kikao cha Jumatatu cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) ya madai hewa kwamba Iran inapeleka silaha nchini Yemen, kwamba: 

kilichotokea kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ni usanii mchafu ulioonyeshwa kwa lengo la kuiunga mkono nchi iliyoanzisha uvamizi dhidi ya Yemen.

Mohammad Javad Zarif ameyasema hayo jana usiku mbele ya waandishi wa habari mara baada ya kuwasili nchini Bulgaria na kuongeza kwamba: Marekani na washirika wake wamezusha tuhuma hewa dhidi ya Iran ili kuficha jinai zao wanazofanya nchini Yemen.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amebainisha kwamba tangu ulipoanza mgogoro nchini Yemen, Tehran imekuwa ikisisitiza kila mara kuwa njia pekee ya kutatua mgogoro huo ni ya "kisiasa" na ndipo ikaandaa na kuwasilisha mpango wa vipengele vinne.
Dakta Zarif amefafanua kuwa mpango huo unatilia mkazo usitishaji vita wa haraka nchini Yemen, kutumwa misaada ya kibinadamu, kufanyika mazungumzo baina ya Wayemen wenyewe kwa wenyewe na kuundwa serikali pana na jumuishi itakayoweza kuwa na uhusiano mzuri na majirani zake.
Itakumbukwa kuwa siku ya Jumatatu, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilifanya kikao kujadili rasimu za maazimio mawili kuhusiana na Yemen.
Rasimu ya azimio la kwanza ilipendekezwa na Uingereza ikiwa na lengo la kuiwekea mashinikizo Iran kufuatia madai kwamba eti inapeleka silaha nchini Yemen; hata hivyo rasimu hiyo ilipigiwa kura ya veto na Russia. 
Uingereza iliandaa rasimu ya azimio hilo kwa msaada wa Marekani na Ufaransa.
Rasimu ya azimio la pili ilipendekezwa na Russia ikiwa na lengo la kurefusha vikwazo vya silaha dhidi ya Yemen hadi Februari 2019. Rasimu ya azimio hilo ilipitishwa kwa kauli moja na wanachama wote 15 wa kudumu na wasio wa kudumu wa Baraza la Usalama.
Tangu mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Imarati (UAE), Marekani, Uingereza na Ufaransa, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa angani, baharini na nchi kavu. 
Uvamizi huo wa kijeshi umesababisha makumi ya maelfu ya raia wa Yemen kuuawa na kujeruhiwa mbali na mamilioni ya wengine waliopoteza makazi yao.
 chanzo:

Comments