WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewahakikishia wananchi wa wilaya ya Misungwi
kuwa vijiji vyote vitapatiwa huduma ya maji safi kupitia miradi
inayotekelezwa katika wilaya hiyo ukiwemo wa Mbarika-Misasi
utakaogharimu sh. bilioni 12.4.
Alitoa
kauli hiyo jana (Jumatatu, Februari 19, 2018) wakati akizungumza na
wananchi mara baada ya kuweka jiwe la ujenzi wa mradi huo akiwa katika
siku ya tano ya ziara yake ya kikazi mkoani Mwanza. Mradi huo
unatarajiwa kuhudumia vijiji 12.
Vijiji
hivyo ni Igenge, Lutalutale, Bugisha, Ngaya, Ikula, Sumbugu, Matale,
Kasololo, Isuka, Nduha, Manawa na Misasi ambapo jumla ya wakazi 47,011
wanatarajiwa kunufaika na mradi huo.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano ina mikakati mizuri inayolenga kumaliza
tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali
nchini vikiwemo vijiji vya wilaya ya Misungwi ili kuwawezesha wananchi
hasa wanawake kushiriki katika shughuli za maendeleo kuliko kutafuta
maji.
Waziri
Mkuu alisema Serikali kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya
kumtua mama ndoo, itahakikisha wananchi katika maeneo yote nchini
wanapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400
kutoka kwenye makazi yao.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Misungwi, Bw. Eliud
Mwaiteleke alisema mradi huo umegawanyika katika miradi midogo minne
ambayo ni Igenge, Mbarika-Ngaya, Ngaya-Matale na Matale-Manawa-Misasi.
Alisema
shughulli zilizokamilika ni pamoja na ujenzi wa vituo 48 vya kuchotea
maji, matanki mapya manne na moja limekarabatiwa pamoja na mtandao wa
mabomba wenye urefu wa kilomita 73,087.
Awali,
Waziri Mkuu aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa shule ya Sekondari ya
Kata ya Gulumungu katika kijiji cha Nyamayinza, ambapo aliwapongeza
wakazi wa kata hiyo kwa uamuzi wa kujenga shule, ambayo itawawezesha
watoto wao kupata elimu.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, FEBRUARI 20, 2018.
chanzo:Mpekuzi.
Comments