
Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amesema
matarajio ya mahakama nchini kuanza kusikiliza kesi kwa kutumia mtandao
ni utaratibu mzuri utakaosaidia kupunguza gharama.
Waziri Kabudi aliyasema hayo jana Januari 31, 2018 jijini Dar es
Salaam wakati akihojiwa na waandishi wa habari kuhusu mpango huo, baada
ya kufungua jengo la Mahakama ya Wilaya ya Kigamboni na kuongeza kuwa
mashahidi watatoa ushahidi wakiwa nje ya mahakama.
“Mimi mwenyewe sikujua kabisa matumizi ya mtandao hata
WhatsApp, nimeanza kutumia hivi karibuni baada ya kuapishwa… teknolojia
yoyote mpya inapokuja ambao ni wagumu kuielewa ni watu wa umri wangu,
lakini kwa vijana wanaelewa kwa haraka zaidi,” alisema.
Waziri alisema kuwa utaratibu huo wa mahakama kuingia kwenye mfumo wa
Tehama utasaidia kupunguza gharama kwa mfano, kesi ikiwa Dar es Salaam
na shahidi yupo Mbeya hatalazimika kusafiri kwa ajili ya kutoa ushahidi.
“Haitatakiwa kutolewa mkoani Mbeya kuja Dar es Salaam kwa
ajili ya ushahidi, atatoa ushahidi wake akiwa Mbeya na jaji ama hakimu
ambaye yupo Dar es Salaam atamuona na kumsikiliza,” alisema.
Aliongezea: “Hata kwa maabusu ambao wapo gerezani kwa
ajili ya kwenda kuahirisha kesi au maombi ya dhamana hana haja tena ya
kwenda mahakamani.”
Hata hivyo, Prof. Kabudi alieleza kuwa kuna haja ya watu kujifunza.
Ni kweli tunahitaji kujifunza zaidi kuhusu matumizi ya mtandao, lakini
umuhimu huo ni kwa watu wenye umri mkubwa kuliko vijana, maana vijana
mtandao anao mkononi,” alisema. Kabudi alisema teknolojia kwa sasa
imesogezwa hadi kwenye simu kwa hiyo mtu anaweza kupata taarifa zake za
kesi.
Alisema baada ya muda Watanzania wengi watafurahia mfumo wa mahakama
kwa njia ya Tehama kwa kuwa kwa sasa miundombinu ipo pamoja na uelewa,
ingawa ni jukumu ya mahakama kuwaelimisha wananchi kuhusiana na
utaratibu huo.
Alisema suala hilo ni muhimu na linaendana na wakati, hivyo ni jambo
zuri kuipongeza mahakama kwani mahakama zinakuwa nyuma kwenye
mabadiliko, lakini kwa Mahakama ya Tanzania imekuwa mbele ya taasisi
nyingi za sheria katika kuleta mabadiliko.
Aidha, aliwataka wananchi wa Kigamboni waitumie mahakama hiyo na kuyatunza majengo hayo ili yadumu kwa muda mrefu.
Chanzo: zanzibar24.
Comments