Kanali ya Televisheni ya al-Masirah imetangaza kuwa, operesheni ya kijeshi ya vikosi vya Yemen katika maeneo ya kaskazini na kusini kwa mji wa Jazan huko Saudia imepelekea kwa akali wanajeshi wanne wa Saudia kuangamizwa.
Aidha operesheni nyingine kama hiyo iliyofanywa katika eneo jingine katika mji wa Jazan nayo pia imepelekea kuangamizwa wanajeshi wengine wanne wa Saudia.
Kuangamizwa kwa wanajeshi hao wa Saudi Arabia kumetokea muda mchache baada ya raia zaidi ya 20 wa Yemen kuuawa katika jinai mpya ya mashambulio ya anga yaliyofanywa na ndege za kivita za Saudi Arabia katika mikoa ya Hajjah na Sa'dah iliyoko kaskazini na kaskazini magharibi mwa nchi hiyo.
Tangu mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea mzingiro nchi hiyo wa angani, baharini na nchi kavu kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abd Rabbuh Mansour Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi.
Saudia na Umoja wa Falme za Kiarabu (Imarati) zinashirikiana katika hujuma na mashambulio yao dhidi ya Yemen, hata hivyo hadi sasa zimeshapata hasara kubwa kutokana na uvamizi ziliofanya dhidi ya nchi hiyo.
Comments