Na: Veronica Kazimoto ,Arusha
Mamlaka
ya Mapato Tanzania (TRA), kwa mara nyingine ndani ya wiki mbili
imekamata na kutaifisha tani moja ya sukari, mafuta ya kupikia katoni 10
na gari lililotumika kusafirisha bidhaa hizo kutoka nchini Kenya
kupitia njia za magendo mpakani Namanga mkoa wa Arusha.
Meneja
Msaidizi wa Forodha mkoani hapo Edwin Iwato alisema bidhaa hizo
zimekamatwa usiku wa kuamkia jana na ni mali ya mfanyabiashara Paul
Swai, ambaye alitumia gari namba T 496 AFE Nissan Carravan mali ya
Christian Nko ambalo limetaifishwa pamoja na bidhaa husika.
"Tumemkamata
mfanyabiashara mwingine aitwae Paul Swai akiwa anaingiza nchini bidhaa
kutoka Kenya kuelekea mkoani Arusha kupitia njia za magendo bila kibali
wala kulipa ushuru wa Serikali", alisema Iwato.
Iwato
amefafanua kuwa tani moja iliyokamatwa ambayo ni mifuko 20 ya sukari
ina thamani ya shilingi 2,200,000 na mafuta ya kupikia ambayo ni
kilogramu 12 yana thamani ya shilingi 520,000.
Mfanyabiashara
huyo pamoja na dereva wa gari lililotaifishwa watachukuliwa hatua kwa
mujibu wa Sheria ya Forodha na bidhaa hizo baada ya kukaguliwa na
kugundulika kuwa zinafaa kwa matumizi ya binadamu zitagawiwa kwa taasisi
mbalimbali za Serikali zenye uhitaji kwa mujibu na taratibu zilizowekwa
na TRA.
Hii
ni mara pili katika mwezi huu ambapo Mamlaka ya Mapato Tanzania
imekamata na kutaifisha bidhaa mbalimbali zikitokea nchini Kenya kupitia
njia za magendo mpakani Namanga mkoa wa Arusha.
chanzo:Mpekuzi.
Comments