SIMBA imeshaondoka kwenda Djibouti kwa ajili ya mchezo wao wa marudiano wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gendermarie Nationale na imekula kiapo kuwa lazima wenyeji wao wapigwe nyingi mapema tu licha ya kwamba watakua kwao.
Wawakilishi hao wa Tanzania wameifuata Gendermarie wakiwa na hazina ya ushindi mnono wa mabao 4-0 walioupata katika mchezo wa kwanza uliopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Kama ulikuwa unadhani Simba imeridhika na ushindi huo wa nyumbani, basi pole yako, kwani kikosi hicho kimesema kinaenda ugenini kutafuta rekodi Afrika na si sifa, hivyo watawavaa Wadjibouti kama wapo katika mechi ya fainali ili washinde.
Tena si kushinda tu, bali washinde kwa kishindo kusudi waingie raundi ya pili kwa heshima kabla ya kuanza kujipanga kuwakabili wapinzani wao watakaovaana nao katika hatua hiyo iwe El Masry ya Misri wanaopewa nafasi kubwa ama Green Buffaloes ya Zambia.
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma na kiungo wa kikosi hicho, James Kotei walisema kwa nyakati tofauti jana Jumapili muda mfupi kabla ya kupanda ndege kuwa hawaendi Djibout ili kushangaa majengo, isipokuwa kushinda mchezo huo tena kwa mabao mengi tu.
Kocha Djuma alisema wana imani ya kupata ushindi mkubwa kwani wanaupa uzito mkubwa mchezo huo ambao baadhi ya mashabiki wao wanauona ni kama wa kukamilisha ratiba tu.
“Tutacheza kwa kushambulia na kujilinda. Tunataka mabao yapatikane zaidi, pia tusiruhusu mabao, tupo mbele kwa mabao manne lakini tunahitaji mabao mengine tukiwa ugenini,” alisema.
Naye Kotei anayeichezea Simba kwa mwaka wa pili sasa, alisema ni mara yake ya kwanza kucheza mashindano hayo, hivyo anataka kujitengenezea rekodi nzuri akiwa na kikosi cha Simba, ili iwe historia nzuri katika maisha yake ya soka.
“Ni mara yangu ya kwanza kushiriki mashindano haya ya kimataifa, naamini nikiwa na Simba tunaweza kutengeneza historia nzuri,” alisema Kotei.
“Kwetu kila mechi ni muhimu, tulishinda hapa lakini tunataka kushinda tena mechi ijayo. Nikiwatazama wapinzani wetu, tuna nafasi kubwa ya kushinda, siyo wagumu sana.
“Simba imerejea kwenye mashindano haya baada ya muda mrefu, ni lazima tuonyeshe kwamba tumekuja kivingine. Tuna timu nzuri, kuanzia nyuma kwenda mbele, kila eneo limekamilika,” alisisitiza kiungo huyo.
KAPOMBE, MANULA NAO
Wakati huo huo, kipa wa Simba, Aishi Manula amefichua kuwa wachezaji wote wanaounda safu ya ulinzi ya kikosi hicho, wamehamasishana kucheza kwa kujitolea ili wasiruhusu bao kwenye mechi hiyo ya marudiano.
“Kuna wakati ambao wachezaji lazima tuhamasishane, hapo tunapata wakati hata wa kuambiana. Mfano safu yetu ya ulinzi inapambana kuona tunafanya kitu chenye manufaa kwa timu hasa kwa kutoruhusu kufungwa,” alisema Manula.
“Hatuwezi kuichukulia poa mechi hiyo, lazima twende tukiwa na akili timamu kwani wapinzani wetu walitusoma staili yetu ya kucheza hivyo hawawezi kucheza kwa kiwango cha chini ama kile walichokionyesha taifa.”
Kwa upande wake, Shomary Kapombe alishauri kila mchezaji kujituma kwa asilimia 100 ili waweze kurejea kifua mbele.
Alifafanua kwamba mabeki wanapaswa kuwajibika ipasavyo, viungo na washambuliaji pia wawe makini.
“Hatuwezi kuchukulia poa mchezo huu, lazima tuwe makini na kila mchezaji akawajibike ipasavyo akijua Watanzania wanahitaji kuona timu zao zinasonga mbele,” alisema.
MAVUGO KAZINGUA
Katika hatua nyingine, Laudit Mavugo, ameachwa katika msafara huo uliondoka jana kutokana na utata wa umri kwani ulioandikwa kwenye pasipoti yake ni tofauti na ule ulio kwenye usajili wake.
Comments