Serikali kutolea mwongozo matamko ya Makonda na Mnyet.

Hatua ya wakuu wawili wa mikoa, paul Makonda na Alexander mnyeti kutoa matamko ya kusimamisha shughuli au kuvunja mabaraza ya kata, Serikali imesema inaandaa mwongozo kuhusu suala hilo.

jumatatu iliyopita, Makonda ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam alitoa tamko la kusimamisha mabaraza hayo katika mkoa wake kabla ya Mnyeti wa Mkoa wa Manyara kutamka kuvunja baraza la Ardhi Kata ya Murray, wilayani Mbulu juzi.

Alipotafutwa jana kuzungumzia hatua ya wakuu hao, katibu Mkuu Ofisi ya Rais (TAMISEMI), Mussa Iyombe alisema, “tunakamilisha mwongozo kuhusu suala hilo wiki hii, fanyeni subira.”

Uamuzi wa Mnyeti
Mnyeti alitangaza uamuzi huo baada ya kupokea malalamiko ya wananchi kunyanyaswa, kuombwa rushwa na kunyimwa haki.

Akizungumza katika Kata hiyo alisema hawezi kuliacha baraza hilo liendelee kufanya kazi ilhali wananchi wananlalamika kukosa haki.

Alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri ya mji wa Mbulu, Anna Mbogo kuanza mchakato wa kupatikana viongozi wapya waadilifu wa baraza hilo la kata ili waendelee kuwatumikia wananchi na kuagiza mikutano ya wananchi kuwachagua wajumbe wengine ianze upya.

“Tafuteni watu waadilifu, wenye weledi na hofu ya Mungu, ambao wanaweza kuwahudumia wananchi ili washike nafasi hizo na kutekeleza majukumu yao ipasavyo,” alisema mnyeti.

Hatua ya Mnyeti ilitokana na malalamiko kutoka kwa mkazi wa Murray, Michael Amme kwamba baraza hilo halitendi haki na wananchi wanyonge wanonewa. amme alidai kwamba familia yake iliporwa eneo kutokana na uamuzi wa barazsa hilo.

Mjumbe wa baraza hilo, Verani Anthony alisema wananchi wanapaswa kupatiwa elimu kuhusu utendaji kazi wa baraza hilo kwa kuwa wao hutekeleza wajibu wao ipasavyo.

Kuhusu Makonda
Juzi, iyombe akizungumza kuhusu tamko la Makonda, alisema mkuu huyo wa mkoa alishatoa ufafanuzi kwa maandishi akikana kusimamisha mabaraza hayo kufanya kazi.

“Tulimtaka atuandikie barua ya kutueleza na tayari ameshafanya hivyo, tumemalizana nae kwa maandishi, hakusimamisha mabaraza hayo kufanya kazi,” alisema Iyombe.

Hata hivyo, katibu mkuu huyo alipoulizwa kama Makonda alitakiwa kuandika barua baada ya kuvunja kipengele kipi cha sheria kutokana na tamko lake, alisema

“Sitaki kusema alivunja kipengee ni wewe wasema, ninachokisema wananchi wakielewe, kulikuwa na maswali watu wanahoji kuhusu suala hilo ndiyo maana tukamtaka atufafanulie na amefanya hivyo kwa maandishi.”

Waraka wa Tume
Andiko la Tume ya Kurekebisha Sheria kwenye mapitio ya mfumo wa utoaji haki katika mashauri ya madai, sehemu ya III la Julai 2012 linalopatikana kwenye mtandao linaelezea utekelezaji wa Sheria ya Mabaraza ya Kata ya mwaka 1985.

Linasema mabaraza hayo yanapaswa kuwa chini ya usimamizi wa Serikali za Mitaa na wajumbe huteuliwa na kamati ya maendeleo ya kata. Baraza huongozwa na mwenyekiti anayeteuliwa na halmashauri husika.

Majukumu ya baraza ni kutunza amani kwenye kata, kutatua migogoro, kusuluhisha ndoa na kusimamia utekelezaji wa sheria ndogondogo kama zilivyopitishwa na halmashauri husika. Baraza pia lina uwezo wa kutatua migogoro yote ya ardhi katika kata, iwe ardhi iliyopimwa au isiyopimwa.

Uteuzi wa viongozi wa mabaraza Kwa mujibu wa sheria, uteuzi wa mwenyekiti wa baraza la ardhi na nyumba la wilaya unafanywa na wizara inayohusika na masuala ya ardhi wakati uteuzi wa wajumbe wa baraza la kata unafanywa na halmashauri husika.

Hata hivyo, katika andiko hilo, Tume ilibaini kuwa vyombo vilivyopewa uwezo wa kuajiri au kufanya uteuzi wa nafasi hizo vina mwingiliano wa kisiasa ambao unaweza kuingilia utendaji kazi wa maofisa wanaowateua au kuwashawishi katika uamuzi wanaoyafanya.

Chanzo: Mwananchi.

Comments