
Hatua hiyo imekuja baada ya ndugu wa binti huyo kususa kupokea mwili
wa mwanafunzi huyo uliokuwa ukifanyiwa uchunguzi Hospitali ya Taifa
Muhimbili (MNH) bila kuelezwa nini kilichomuua.
Wakizungumza mara baada ya maafikiano baina yao na madaktari,
wamesema sehemu ya ripoti ya uchunguzi ambayo wameridhika nayo na sasa
wanakwenda kufanya kikao cha ndugu kujadili namna gani watampumzisha
Akwilina.
Shemeji wa mwanafunzi huyo, Festo Kavishe amesema uchunguzi wa mwili
huo, umeonyesha kwamba Akwilina alijeruhiwa vibaya kichwani.
“Ripoti ambayo tumepewa imeonyesha kwamba kichwa cha
marehemu kilipasuliwa vibaya na risasi ambayo iliingilia upande wa
kushoto kwa kichwa chake na kutokea upande wa kulia ambao umefumuka
vibaya,”amesema.
Kwa mujibu wa Kavishe, iwapo madaktari wasingewapatia majibu hayo
wasingethubutu kuuchukua mwili huo kwa mazishi, kwa sababu walihitaji
kupata picha kamili ya nini kilimuua Akwilina.
“Sasa tumeshafahamu nini hasa kimemuua ndugu yetu kwa
mujibu wa ripoti iliyotolewa na madaktari baada ya uchunguzi, hivi sasa
tunakwenda kujadiliana kuhusu mazishi yake,” amesema Kavishe.
Akwilina alifariki dunia Februari 16, 2018 baada ya kupigwa risasi
kichwani akiwa kwenye daladala wakati polisi wakiwatawanya waandamanaji
ambao ni wafuasi wa Chadema.
chanzo: zanzibar24.
Comments