Ripoti: 85% ya Wamarekani hawana imani na Kongresi.

Ripoti: 85% ya Wamarekani hawana imani na Kongresi Utafiti mpya wa maoni unaonyesha kuwa Wamarekani wengi hawana imani na Kongresi ya nchi hiyo wakisisitiza kuwa bunge hilo linatumikia maslahi ya makundi ya kulobi na wala sio wananchi wa kawaida.

Utafiti huo uliofanywa na kituo cha utafiti cha NORC na matokeo yake kuchapishwa na shirika la habari la Associated Press unaonyesha kuwa, asilimia 85 ya Wamarekani hawakubaliana na utendakazi wa Bunge la Kongresi.
Matokeo ya utafiti huo uliofanywa kati ya tarehe 15 na 19 mwezi huu wa Februari yamebainisha kuwa, asilimia 89 ya wafuasi wa chama cha Democratic na asilimia 82 ya Warepulican hawaridhishwi kabisa na utendaji wa bunge hilo.
Thuluthi moja ya Wamarekani walioshirikishwa kwenye utafiti huo wamesisitiza kuwa, wawakilishi wao katika Kongresi ya nchi hiyo wameshindwa kupasisha sheria za maana zinazowahusu wananchi wa  kawaida.
Kadhalika utafiti huo umesema asilimia 66 ya wananchi wa Marekani wanaamini kuwa Bunge la nchi hiyo linatoa kipaumbele kwa makundi ya kulobi, kama vile Chama cha Wamiliki wa Bunduki nchini humo.
Utafiti mwingine wa maoni uliofanywa hivi karibuni na shirika la Gallup ulionyesha kuwa, ni asilimia 20 tu ya Wamarekani ndio wanaoridhika na kazi ya Kongresi, huku asilimia 38 wakiwa na imani na utendakazi wa Rais Donald Trump wa nchi hiyo.
 chanzo:parstoday.

Comments