Rais Shein azungumza na Balozi wa Nigeria nchini Tanzania.

Image result for dr sheinRAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ameipongeza Serikali ya Nigeria kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu na kueleza haja ya kuendelea na hatua hiyo kwa sekta nyengine ili kuzidisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria uliopo kati ya Zanzibar na nchi hiyo. 
Akizungumza na Balozi mpya wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Sahabi Isa Gada Ikulu mjini Zanzibar,  Dk. Shein alieleza kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya  Nigeria na Zanzibar una historia kubwa kwani nchi hiyo ni miongoni mwa nchi za mwanzo zilizoiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu mara tu baada ya Mapinduzi matukufu ya mwaka 1964.
Katika Mazungumzo hayo, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa hatua ya ujio wa walimu 16 hapo kesho kutoka nchini Nigeria kwa ajili ya kuja kusomesha skuli za Sekondari za Zanzibar ni ushahidi mzuri wa kuonesha kuimarika kwa uhusiano na ushirikiano kati ya pande mbili hizo.
Aidha, Dk. Shein alimueleza Balozi Gada haja ya kuendeleza mahusiano na ushirikiano kupitia vyuo vikuu vya Nigeria na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) hatua ambayo itasaidia kubadilishana uzoefu na utaalamu katika ngazi ya vyuo vikuu na kusema wanawakaribisha wawekezaji kutoka Nigeria kutokana na Zanzibar kuwa na rasilimali za kutosha.
Alisisitiza kuwa kwa vile tayari wawekezaji wa nchi hiyo akiwemo muekezaji aliyewekeza kiwanda cha saruji katika maeneo ya Kusini mwa Tanzania hivyo, ni vyema Ubalozi huo ukaitangaza Zanzibar kwa waekezaji wa nchi hiyo ili waje kuwekeza katika sekta  nyengine vikiwemo viwanda vya uvuvi.
Dk. Shein pia, alisisitiza haja ya mashirikiano katika sekta ya sanaa na utamaduni kati ya Zanzibar na Nigeria hasa ikizingatiwa kuwa tayari nchi hiyo imepiga hatua katika sekta hiyo ikiwa ni pamoja na kujiimarisha katika masuala ya filamu na maigizo kupitia kiwanda cha uigizaji filamu cha nchi hiyo Nollywood ili Zanzibar nayo iweze kuwa na kiwanda kama hicho.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza haja ya kuwepo mashirikaino kwa wananchi na wa pande mbili hizo kutembeleana kwa lengo la kukuza uhusiano na ushirikiano uliopo sambamba na kuiimarisha sekta ya utalii kati ya Zanzibar na Nigeria huku akipongeza hatua za kuendelea kuimarika kwa uchumi wa Nigeria.
Nae Balozi mpya wa Nigeria katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Sahabi Isa Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya pande mbili hizo si mpya bali ni wa muda mrefu hivyo aliahidi kuwa nchi yake itauimarisha.
Dk. Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa walimu 16 wa Sekondari wa Sayansi wanatarajiwa kuwasili nchini hapo kesho wakitoa Nigeria ikiwa ni hatua moja wapo ya kuendeleza uhusiano na ushirikiano uliopo kati ya Zanzibar na nchi hiyo.
Aidha, Balozi huyo alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa juhudi za makusudi zitaendelea kuchukuliwa na Ubalozi wake katika kuhakikisha idadi hiyo ya walimu inaongezeka ili kutoa nafasi nzuri ya kuimarika kwa sekta ya elimu hapa Zanzibar.
Sambamba na hayo, Balozi Gada alimueleza Rais Dk. Shein kuwa suala zima la kuwakarisha waekezaji kuja kuekeza Zanzibar atalifanyia kazi kwa kutambua kuwa wapo waekezaji wengi katika sekta hiyo nchini mwake hasa ikizingatiwa kuwa Nigeria nayo ina uzoefu katika sekta ya uvuvi.
Katika ujio wa walimu wa Sayansi kwa ajili kusomesha Skuli za Sekondari hapa Zanzibar kutoka nchini Nigeria, idadi yao mara hii ni walimu 50 na wote ni walimu wa masomo ya Fizikia na Hesabati ambapo tayari wameshafika walimu 8 na kesho wanatarajiwa kuwasili nchini walimu 16 na watakaobaki ambao jumla yao ni  26 watakuja hapo baadae, walimu hao hufundisha kwa muda wa miaka miwili miwili.
chanzo:Zanzibar24.

Comments