PAMOJA na Simba kupunguzwa kasi Ligi Kuu Bara jana Alhamisi kwa sare ya mabao 2-2 mbele ya Mwadui, mastaa wake, Emmanuel Okwi na John Bocco, wamethibitisha kwamba msimu huu moto wao hauzimiki.
Bocco ambaye amejiunga na Simba msimu huu akitokea Azam, alifunga bao lake la 10 katika dakika ya tisa tu ya mchezo huo wa ugenini huku Okwi akitoa gundu la kutofunga nje ya Dar es Salaam baada ya kupachika kimiani penalti murua katika dakika ya 71.
Simba ilipunguzwa kasi baada ya Mwadui kusawazisha mabao yote mawili, akianza David Luhende kwa mpira wa adhabu dakika ya 60 kisha Paul Nonga kufunga kwa kichwa dakika moja tu kabla ya mchezo kumalizika.
Matokeo hayo yameifanya Simba iendelee kusalia kileleni ikiwa sasa na pointi 42 huku wapinzani wao Yanga walioichapa Majimaji mabao 4-1 juzi Jumatano, kujikita nafasi ya pili na pointi 37. Mwadui imepanda hadi nafasi ya 10 ikiwa na alama 19.
Habari kubwa mjini Shinyanga iliendelea kuwa Bocco na Okwi ambao sasa kwa pamoja wamefunga mabao 24 Ligi Kuu na kuwa pacha iliyofunga zaidi msimu huu.
Kipa wa Simba, Aishi Manula, alitibuliwa rekodi yake ya kucheza mechi saba mfululizo sawa na dakika 630 bila kuruhusu bao baada ya kufungwa mabao hayo mawili hiyo jana.
Katika mchezo huo, Mwadui walikosa nafasi mapema tu ambapo Jerome Mgeveke alishindwa kumalizia krosi ya Nonga na dakika ya tisa Bocco aliwainua mashabiki wa Simba kwa bao murua la kuongoza akiunganisha faulo ya Said Ndemla.
Simba ilipata pigo katika dakika ya 29 baada ya Bocco kuumia hivyo kufanya mabadiliko ya lazima ya kumpa nafasi Laudit Mavugo ambaye hata hivyo hakumaliza mchezo huo, kwani baadaye naye alitolewa.
Simba ilitaka kujihakikishia ushindi mapema lakini shuti kali la Shomary Kapombe katika dakika ya 11 lilipanguliwa na kipa wa Mwadui, Anorld Masawe, aliyeonyesha kiwango maridadi kwenye mchezo huo.
Mpira ulitulia na timu zote kushambuliana kwa zamu, lakini Mwadui ilipoteza nafasi ya wazi katika dakika ya 32 ambapo kipa wa Simba, Aishi Manula, alifanya juhudi binafsi kumzuia mshambuliaji, Miraji Athuman, aliyewatoroka mabeki wa Msimbazi na kutaka kupeleka kilio langoni mwao.
Pamoja na Simba kuzidisha kasi ya mashambulizi yake, Masawe alithibitisha kwamba ubora wake umezidi kuongezeka baada ya kupangua shuti kali la Okwi katika dakika ya 37 kabla ya Awadhi Juma kupoteza nafasi ya kuisawazishia Mwadui dakika nne baadaye.
Simba ilikwenda mapumziko ikiwa kifua mbele, lakini David Luhende aliisawazishia timu yake katika dakika ya 60 kwa faulo iliyokwenda moja kwa moja wavuni na kumuacha kipa wa Simba, Manula akiwa hana cha kufanya.
Okwi ambaye tangu msimu uanze alikuwa hajafunga bao lolote nje ya Dar es Salaam, alitoa gundu katika dakika ya 71 kwa mkwaju wa penalti baada ya awali kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki Mgeveke.
Simba ilipata pigo katika dakika ya 84 baada ya beki wake, Juuko Murshid, kuonyeshwa kadi ya pili ya njano iliyozaa nyekundu jambo lililolazimisha wapambane na hali yao katika dakika sita zilizokuwa zimesalia na zile tano za nyongeza.
Kufuatia kupunguzwa kwa Juuko, kocha wa Simba, Pierre Lechantre alimtoa Mavugo katika dakika ya 87 na kumpa nafasi Paul Bukaba lakini mabadiliko hayo ni kama yalikuwa na gundu kwani dakika mbili baadaye Paul Nonga aliifungia Mwadui bao la kusawazisha akiunganisha krosi ya Luhende.
chanzo:Mwanansport.
Comments