KIPA wa Mwadui FC, Anorld Massawe, ameweka wazi kwamba washambuliaji Ibrahim Ajibu wa Yanga, Emmanuel Okwi wa Simba na Shaaban Idd Chilunda wa Azam ni habari nyingine na ukizubaa tu lazima wakutikise.
Massawe alisema amekutana na washambuliaji wengi katika mechi za Ligi Kuu Bara, lakini watatu hao walimpa changamoto kubwa kutokana na usumbufu wao ndani ya dakika 90 za mechi zao walizokutana msimu huu.
Massawe ambaye ni tunda la kituo cha vijana cha Azam FC, alisema kuwa amecheza mechi za timu kubwa zote na amekutana na changamoto kubwa, lakini timu ambayo ilimpa changamoto zaidi ni Simba japa walitoka sare ya mabao 2-2.
“Kwanza Simba, Yanga na Azam ni timu kubwa katika ligi yetu, zina wachezaji wa kimataifa wengi na wazuri, lakini hata wa hapa nyumbani wapo wachezaji wazuri pia. Mfano Yanga ina Ajibu, ni mchezaji hatari na akiwa na mpira anaweza kufanya lolote, yaani ukizubaa kidogo kakuliza,” alisema.
“Simba pia yuko Emmanuel Okwi, ni hatari sana kwa kuchungulia makipa. Kwa upande wa Azam yupo Shaaban Idd, ni mdogo ila ni hatari, anasumbua mabeki na ana uwezo wa hali ya juu,” alibainisha kipa huyo.
Mwadui inayokamata nafasi ya 10 kwa alama 19 baada ya mechi 18, leo Jumatatu itashuka Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kuvaana na Prisons katika mechi yao nyingine ya ligi kukamilisha raundi ya 19 ya ligi hiyo inayoongozwa na Simba kwa pointi 42.
Comments