Waziri
wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amezindua kiwanda
cha Inhemeter ambacho kitakuwa kinazalisha mita za luku na kuziuza kwa
mashirika ya ugavi wa umeme nchini.
Kiwanda
hicho ambacho ni cha kwanza kujengwa hapa nchini na cha nne Afrika kina
soko la uhakika la kuuza mita 500,000 kwa mwaka kwa Shirika la Umeme
nchini (Tanesco), Wakala wa Umeme Vijijini (Rea) na Shirika la Umeme
Zanzibar (Zeco).
Mwijage
aliyataka mashirika hayo kutumia fursa ya kuwepo kwa kiwanda hicho
kuboresha huduma zao huku akisisitiza kwamba kitakuwa na manufaa mengi
ikiwemo ajira kwa vijana 100 na mashirika kutotumia fedha za kigeni
kuagiza mita nje ya nchi.
“Ninamuomba
mwekezaji kuzalisha bidhaa nyingi zenye ubora wa kimataifa na bei nafuu
sokoni,” alisema Mwijage wakati akizindua kiwanda hicho jijini Dar es
Salaam mwishoni mwa wiki.
Alisema
Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kujenga uchumi wa kati na viwanda
ifikapo 2025 na kuzinduliwa kwa kiwanda cha Inhemeter ni uthibitisho
kuwa azma hiyo imeshaanza kutekelezwa kwa vitendo.
“Tunahitaji
viwanda vitakavyo mpunguzia gharama mlaji au mtuamijia pamoja na
kuzalisha ajira kwa vijana wetu,” alisema huku akitaka aliye tayari
kuanzisha kiwanda ofisi yake iko wazi kumsaidia.
Waziri Mwijage alimpongeza mwekezaji huyo kwa uamuzi wake wa kuja Tanzania.
“Wakati
umefika wa kuondokana na uchuuzi. Tunataka tuzalishe wenyewe hapa
nchini na tuuze nje, simaanishi kuwa hatuhitaji bidhaa za nje, zije zile
tu zenye ubora stahili,” alisema.
Pia alisema anayo furaha kushuhudia uzinduzi wa kiwanda kipya cha 3,307 katika kipindi kifupi.
Awali,
akizungumza kwenye hafla hiyo, Mshauri Mkuu wa kiwanda hicho ambaye pia
ni katibu mkuu mstaafu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk
Adelhem Meru alivishauri vitengo vya manunuzi nchini kusaidia ujenzi wa
viwanda.
“Ningependa
kutoa wito kwa vitengo vya manunuzi kuunga mkono kwa dhati azma hii ya
Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga uchumi wa kati na viwanda.
Ninafahamu vitengo hivi vina nafasi nzuri sana,” alisema.
Kwa
upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Abraham Rajakili
alisema Inhemeter ni kampuni yenye uzoefu wa miaka 20 katika tafiti,
uzalishaji na usambazaji wa mita za luku na tayari wameshasambaza katika
zaidi ya nchini 60 dunia.
“Kiwanda
hiki kitakuwa na uwezo wa kuzalisha mita za luku milioni moja kwa mwaka
na pia kuajiri mafundi mia moja Watanzania,” alisema.
chanzo:Mpekuzi.
Comments