Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam imemhukumu kwenda jela
jumla ya miaka 93 aliyekuwa mfanyakazi wa CRDB, Gura baada ya kumkuta na
hatia ya makosa 29 ya kughushi na mawili ya wizi wa Sh. milioni 29.8 za
benki hiyo.
Aidha,
mahakama hiyo imemtia hatiani Gura kwa kosa la kutakatisha Sh. milioni
29.8 na kumwadhibu kulipa faini ya Sh. milioni 100.
Mahakama
ilisema akishindwa kulipa faini hiyo atakwenda jela kutumikia kifungo
cha miaka mitano na imeamuru arejeshe fedha hizo kwa benki hiyo, na
akishindwa kitatolewa kibali cha kifilisiwa mali zake.
Hukumu hiyo ilisomwa jana na Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba.
Hakimu
Simba alisema mahakama yake imemtia hatiani kwa makosa 32 na kwamba kwa
kosa la pili hadi la 30 mshtakiwa atakwenda jela kutumikia kifungo cha
miaka mitatu kwa kila kosa.
Pia,
alisema Hakimu Simba, mshtakiwa atatumikia kifungo cha miaka mitatu kwa
kosa la 31 na 32 ya wizi wa Sh. 29,889,191 mali ya benki ya CRDB.
Kabla ya hukumu hiyo, mshtakiwa Gura alipewa nafasi ya kujitetea, ili apunguziwe adhabu.
Gura alidai kuwa amekaa mahabusu kwa miaka mitatu, ni mwenye familia ya mke na watoto watatu wote wadogo na wenye kumtegemea.
"Mheshimiwa
hakimu mimi ni mgonjwa nasumbuliwa na marathi ya mgongo, shinikizo la
damu na sukari," alisema Gura. "Maradhi haya yananifanya nisiweze
kusimama kwa muda mrefu. Naiomba mahakama iniangalie kwa jicho la
huruma."
Hakimu Simba alisema adhabu hizo za kifungo jela zitakwenda sambamba na kwamba mahakama imezingatia maombi ya mshtakiwa.
Katika kesi hiyo Gura anadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Agosti,2014 na 2015.
chanzo:Mpekuzi.
Comments