Mbao FC, Kagera kitaeleweka VPL.

MBAO FC imesema hasira ilizonazo za kupoteza mechi zake mbili mfululizo, leo Jumapili itazimalizia kwa Kagera Sugar kuhakikisha wanashinda na kujiweka nafasi nzuri kwenye msimamo wa Ligi Kuu.
Timu hiyo ilichezea vichapo viwili mfululizo dhidi ya Stand United kwa bao 1-0, kisha kuchapwa mabao 2-0 dhidi ya Ruvu Shooting ugenini na leo itakuwa CCM Kirumba kuwakaribisha Kagera Sugar.
Kocha Msaidizi wa Mbao, Ahmad Ally alisema kuwa kupoteza mechi mbili mfululizo kumewachanganya, hivyo leo lazima Kagera Sugar walale mapema.
Alisema makosa waliyoyafanya kwenye mechi hizo, hawatarajii yajirudie tena na wanahitaji pointi tatu ili kujiweka nafasi nzuri katika msimamo.
“Ni mchezo mgumu lakini muhimu sana katika kuuanza mzunguko wa pili,tuna hamu sana ya ushindi baada ya kuukosa mechi mbili mfululizo, hivyo tutapambana hadi tushinde” alisema Ally.


Kocha huyo aliongeza wachezaji wote wapo fiti na hakuna wa kukosa mpambano huo na kutamba kuwa wamejiandaa kikamilifu kubaki na alama tatu.

Comments