Mashindano ya Taifa ya riadha yafutwa.

Katibu Mkuu w Shirikisho la Riadha Tanzania (RT) Wilhelm Gidabuday amesema mashindano ya Taifa ya mbio za Nyika yaliyokuwa yafanyike Februari 24 mwaka huu Mkoani Kilimanjaro hayatafanyika tena.
Gidabuday alisema kuna sababu nyingine zilizosababisha RT kuacha kuyafanya mashindano hayo moja wapo ni kutokana na kukabiliwa na mashindano mengi kwa wakati mmoja.
“Siyo lazima kuyafanya mashindano hayo mwaka huu kutokana na maandalizi ambayo tumeyalenga kwa nguvu nyingi ambapo wanariadha wetu tumewaandaa hasa kwaajili ya Jumuiya ya Madola pamoja na mashindano ya Dunia ya nusu Marathon” alisema Gidabuday.
Pamoja na hilo alisema kuwa mashindano hayo yameshindwa kufanyika kutokana na Shirikisho kutokuwa na fedha za kuandaa mashindano yote yanayowakabili.
Kutokana na kushindwa kufanya mashindano hayo pia Tanzania haitapeleka wawakilishi kwenye mashindano ya Nyika ya Afrika yatakayofanyika Machi 17, nchini Algeria.
“Hakuna athari yoyote kwa kutofanya mashindano hayo wala kutokwenda kushiriki mashindano ya Afrika kwa kuwa mwaka huu sio kalenda ya mashindano ya Nyika ya Dunia ambayo yangetulazimu kushiriki kama tulivyofanya mwaka jana nchini Uganda”


Gidabuday aliongeza kuwa hata mwaka jana mashindano ya Taifa hayakufanyika licha ya kalenda ya IAAF kuwataka kufanya hivyo lakini ripoti iliyopelekwa IAAF ilieleza sababu za msingi za kutofanya mashindano hayo.

Comments