Katika taarifa Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Palestina katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, limetangaza kuwa: "Orodha eti ya ugaidi ya Marekani, kimsingi ni orodha ya Wapinzani wa sera zilizo dhidi ya ubinadmau za Marekani na pia ni orodha ya wanaopambana dhidi ya ughasibu wa Wazayuni na jinai zao."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, uamuzi ulio dhidi ya ubinadamu wa Marekani na njama zilizofeli dhidi ya mapambano ya Palestina ni kielelezo cha wazi cha namna Shetani Mkubwa, yaani Marekani, anavyoshirikiana na utawala wa Kizayuni wa Israeli na kupuuza haki za taifa la Palestina.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, " Hatua hiyo ya Marekani haina maana, ni ya kinafiki na pia ni ya kidhalimu ambayo imechukuliwa dhidi ya taifa la Palestina baada ya madai kuwa eti Quds Tukufu (Jerusalem) ni mji mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel".
Hali kadhalika taarifa hiyo imesema uamuzi wa Marekani wa kumuweka Ismail Haniya katika orodha yake eti ya magaidi ni uamuzi ambao si tu kuwa hautakuwa na taathira hasi katika mapambano bali hata utafichua zaidi taswira halisi ya kigaidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel.
Aidha uamuzi huo pia utaimarisha irada ya viongozi wa harakati za mapambano ya Kiislamu katika kukabiliana na utawala bandia wa Israel.
Taarifa hiyo ya Kongamano la Kimataifa la Kuunga Mkono Palestina katika Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu, Bunge la Iran, pia imetoa wito kwa mabunge yote ya nchi za Kiislamu na zinazojitegemea duniani na pia makundi yote ya kutetea haki za binadamu na uadilifu, na makundi ya mapambano halali dhidi ya Wazayuni kuungana katika kulaani uamuzi huo wa Marekani na ugaidi wa kiserikali wa utawala wa Kizayuni sambamba na kutetea haki za taifa linalodhulumiwa la Palestina.
chanzo:parstoday
Comments