Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe.Samia Suluhu Hassan
amewahakikishia wananchi wa Mkoa wa Simiyu kuwa Serikali itamaliza
kabisa tatizo la uhaba wa dawa za kuuwa wadudu waharibifu wa zao la
pamba.
Mhe.
Makamu wa Rais ameyasema hayo jana wakati akizungumza na wananchi wa
Wilaya ya Busega kwenye Mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Lamadi
wakati akiwa katika siku ya kwanza ya ziara yake Mkoani Simiyu.
Amesema
awamu ya kwanza ya dawa zimeshafika Simiyu kwa ajili ya kuwagawia
wakulima wa pamba na akaahidi kuwa awamu ya pili ya kuleta dawa hizo
inamalizika katika wiki iliyoanza jana tarehe 19/02/2018, hivyo tatizo
hilo litakuwa limekwisha.
“Ninajua
kuna kiasi kikubwa cha dawa kinakuja Simiyu dawa itakuwa nyingi na
wakulima wote watapata, hatuwezi kuacha nguvu zenu zipotee bure na kwa
kuwa Simiyu ni mkoa wa Viwanda na ndiyo unazalisha pamba kwa wingi
tutajenga viwanda vinavyotumia pamba, kwa maana hiyo hatuwezi kuiacha
pamba iharibike” alisema.
Katika
hatua nyingine Mhe.Makamu wa Rais wakati akizungumza na wananchi katika
Kijiji cha Masanzakona baada kuweka jiwe la msingi mradi wa maji wa
Kiloleli amewahimiza wananchi kuchangia huduma za maji ili miradi ya
maji iwe endelevu.
Alisema
Serikali imedhamiria kumaliza kabisa tatizo la maji hapa nchini kwa
kujenga miradi ya maji hivyo ni vema wananchi wakaunga mkono juhudi za
Serikali kwa kuchangia huduma za maji ili kusaidia miradi hiyo
kujiendesha.
Akiwasilisha
taarifa ya mradi wa Kiloleli kwa Makamu wa Rais, Mhandisi wa Maji
Wilaya ya Busega, Mohammed Said alisema mradi huo utagharimu jumla ya
shilingi bilioni 1.6 mpaka kukamilika kwake mwezi Machi 2018 na
utawahudumia wananchi wa vijiji vitatu vya Yitwimila B, Ihale na Ijitu.
Akizungumza
kwa niaba ya wananchi wa Jimbo la Busega, Mbunge wa Busega Mhe. Raphael
Chegeni alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Mhe.Dkt.John Pombe Magufuli kwa kutekeleza ahadi aliyoitoa kwa wananchi
wakati wa kampeni ya kuwapelekea mradi wa Maji wananchi wa kata ya
Kiloleli.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan
ameanza ziara ya kikazi ya siku nne(04) mkoani Simiyu, ambapo amepata
fursa ya kuzungumza na wananchi pamoja na kukagua miradi mbalimbali ya
maendeleo katika Wilaya ya Busega na Bariadi.
chanzo:Mpekuzi.
Comments