Kufutwa kazi makamanda wa juu wa jeshi nchini Saudia; matokeo ya vita vya madaraka na kushindwa kijeshi Aal Saud.

Kufutwa kazi makamanda wa juu wa jeshi nchini Saudia; matokeo ya vita vya madaraka na kushindwa kijeshi Aal Saud Jumatatu ya juzi tarehe 26 Februari, Mfalme wa Saudi Arabia, Salman bin Abdu Aziz aliendelea kufanya mabadiliko ya nyadhifa za juu za uongozi nchini humo ambapo aliwafuta kazi maafisa kadhaa wa ngazi za juu jeshini.

Mabadiliko hayo yamewakumba Mkuu wa Majeshi Jenerali Abdul Rahman bin Saleh al-Bunyan, Mkuu wa Kikosi cha Jeshi la Anga Muhammad bin Awadh Sahim na Meja Jenerali Fahad bin Turki bin Abdul Aziz ambaye alikuwa Kamanda Mkuu wa Kikosi cha Nchi Kavu.
Kufutwa kazi makamanda wa ngazi za juu katika jeshi la Saudi Arabia kunaweza kutathminiwa katika engo na pande kadhaa. Katika miezi ya hivi karibuni na katika fremu ya kile kinachotajwa na weledi wa masuala ya kisiasa kama mapinduzi baridi ya Mfalme Salman, Saudi Arabia imekuwa ikishuhudia wimbi la kufutwa kazi maafisa wa ngazi za juu wa kisiasa, kijeshi na kiusalama. 
Miongoni mwa sababu za mabadilikko hayo ni wasiwasi mkubwa wa familia ya Salman bin Abdul Aziz juu ya uwezekano wa kupokonywa hatamu za uongozi ukiwemo uwezekano wa kutokea mapinduzi ya kijeshi katika fremu ya vita vya kugombania madarakani katika familia ya Aal Saud.
Suala la vita vya kuwania madarakani ni miongoni mwa sifa maalumu za Aal Saud na huu ni ukweli ambao hata ripoti za televisheni za Magharibi zimeukiri bayana.
Hivi karibuni Kanali ya Televisheni ya BBC ya Uingereza ilieleza katika kipindi chake cha matukio ya kweli kilichokuwa na anwani ya "Aal Saud, familia iliyoko vitani" na kuzungumzia ufisadi mkubwa na mivutano ya kuwania madarakka inayoshuhudiwa katika familia hiyo. 
Saad al-Faqih ambaye ni mpinzani wa Saudia anasema katika sehemu moja ya kipindi hicho kwamba: 
Watu wa familia ya kifalme ya Aal Saud wanaishi maisha ya kujiabudu na wamekumbwa na hali ya kujiona ambapo fikra na mtazamo kama huu umewafanya wachukue hatua za kuhodhi madaraka.
Katika mazingira kama haya, hatua ya Mfalme Salman ya kumchagua mwanawe, Muhammad bin Salman, kuwa mrithi wa kiti cha ufalme ni jambo ambalo lilishadidisha vita vya kuwania madaraka nchini Saudia. Wasiwasi umeongezeka zaidi kutokana na kuwa, operesheni za kufuta kazi viongozi wa ngazi za juu na kuteuliwa wengine wapya nchini Saudia hazijaishia katika nyadhifa za kisiasa, bali sekta za usalama na jeshi nazo zimekumbwa na fagio hilo la Mfalme Salman. 
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hatua hizo za Mfalme Salman zinaonyesha wasiwasi mkubwa wa mfalme kwa harakati za lobi mbalimbali ndani ya ukoo huo ambazo hazijafurahishwa na hatua yake ya kukiuka ada ya kijadi ya namna ya kupasiana madaraka.
Mfalme Salman anahofia kwamba, harakati hizo zinaweza kufanya mapinduzi. Mtoto wa Mflame Salman yaani Muhammad bin Salman amechaguliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudia katika hali ambayo kwa mujibu wa hati na wasia wa Mfalme Abdul Aziz, mwasisi wa utawala wa ukoo wa Aal Saud ni kuwa, madaraka yanapaswa kutoka kwa kaka mtu kwenda kwa kaka na madhali watoto wake wangali hai, basi hatamu za uongozi hazitakifikia kizazi cha tatu. Utawala wa Aal Saud ulichukua hatamu za uongozi nchini Saudia mwaka 1932 na katika kipindi chote hiki daima suala la vita vya madarakani limekuwa jinamizi linaloukaba koo utawala huo.
Jambo jingine muhimu ambalo lililikuwa na taathira katika kuuzuliwa na kufutwa kazi makamanda wa jeshi nchini Saudia ambalo kimsingi ndio sababu halisi ya mabadiliko hayo makubwa katika jeshi, ni kushindwa mtawalia utawala wa Aal Saud katika medani ya kijeshi Mashariki ya Kati. 
Katika miezi ya hivi karibuni walimwengu wameshuhudia Saudia ikiangukia pua na kushindwa katika siasa zake za kupenda vita huko Yemen baada ya vikosi vya majeshi yake kuchezea vipigo kutoka kwa wanamapambano na wananchi wa Yemen.
Samih Askar, mchambuzi wa masuala ya kisiasa wa Misri anasema kuwa: Utawala wa Aal Saud umeshindwa kisiasa, kijeshi na kimaadili katika vita vyake dhidi ya wananchi wa Yemen. 
Tangu mwezi Machi mwaka 2015, na kwa msaada na uungaji mkono wa Marekani, Saudi Arabia ilianzisha uvamizi wa kijeshi dhidi ya Yemen na kuiwekea nchi hiyo mzingiro wa angani, baharini na nchi kavu kwa kisingizio cha kutaka kumrejesha madarakani kibaraka wake, Abd Rabbuh Mansour Hadi, rais wa nchi hiyo aliyejiuzulu na kuitoroka nchi.
Hata hivyo kinyume kabisa na matarajio ya viongozi wa Saudi ambao walikuwa wakidhani kwamba, kwa muda mfupi wangeweza kufikia lengo hilo, hivi sasa ni karibu miaka mitatu na inaonekana Saudia imekwama katika kinamasi cha vita hivyo. Mabadiliko na matukio ya mara kwa mara ya viongozi wa Saudia hususan kubadilishwa maafisa wa masuala ya kijeshi na kiusalama ni mambo ambayo kwa hakika yanaonyesha hali ya kuchanganyiwa iliyoukumba utawala wa Aal Saud mbele ya muqawama wa wananchi wa Yemen ambao wamesimama kidete kukabiliana na uvamizi dhidi ya nchi yao.
chanzo:parstoday.

Comments