Jeremy Corbyn amesema hayo katika msikiti wa Finsbury kaskazini mwa London katika kampeni ya nchi nzima nchini Uingereza inayoendeshwa na Waislamu na ambayo inajulikana kwa jina la "Tembeleeni Misikiti" na kubainisha kwamba, uhalifu unaofanywa kwa sababu ya chuki dhidi ya Uislamu unatia aibu.
Kiongozi huyo wa chama cha Leba ameshambulia vikali kampeni chafu ya chuki dhidi ya Uislamu na kubainisha kwamba, akthari ya wananchi wa Uingereza hawakubaliani na jambo hilo.
Jeremy Corbin amesisitiza kuwa, katika vikao ambavyo amewahi kufanya na Waislamu hususan wanawake ambao wamekuwa wakivunjiwa heshima kutokana na kuvaa vazi la Hijabu, amewataka warekodi video wakati uhalifu huo unapofanyika na kuwasilisha mashtaka katika vyombo vya sheria.
Kiongozi huyo wa chama cha Leba ameeleza kuwa, njia na majibu bora kabisa ya kukabiliana na vitendo hivyo ni wananchi kuwa na umoja na mshikamano.
Zaidi ya misikiti 200 nchini Uingereza imeshiriki katika kampeni hiyo ya "Tembeleeni Misikiti" na lengo la mpango huo ni kuwafahamisha wafuasi wa dini nyingine kuhusu mafundisho ya Uislamu na wakati huo huo kukabiliana na kampeni chafu ya chuki dhidi ya Uislamu.
Kituo cha Kiislamu cha Uingereza kilicho chini ya ofisi ya Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu nacho kimeshiriki katika kampeni hiyo ya "Tembeleeni Misikiti".
Comments