Indhari ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi nchini Myanmar.

Indhari ya Umoja wa Mataifa kuhusiana na kuendelea mauaji ya kizazi nchini MyanmarKamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametahadharisha kuhusiana na matokeo mabaya ya kuendelea mauaji ya kizazi yanayofanywa na serikali ya Myanmar dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya katika nchi hiyo.

Zeid Raad al-Hussein, Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesisitiza katika safari yake huko Jakarta mji mkuu wa Indonesia kwamba, hatua kama za mauaji ya umati na kutaka kuangamiza kizazi zinazofanywa dhidi ya Waislamu wa jamii ya Rohingya wa nchini Myanmar ni mambo ambayo yanaweza kuibua mapigano ya kidini ambayo yatavuka mipaka ya nchi hiyo na kuenea katika nchi nyingine. 
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, nchi ya Myanmar inakabiliwa na mgogoro mkubwa ambao umekuwa na taathira mbaya kwa usalama wa eneo hilo.
Wasiwasi kuhusiana na hali ya Waislamu wa Rohingya imeongezeka zaidi baada ya kugunduliwa makaburi matano ya umati katika mkoa wa Rakhine. 
Katika makaburi hayo kulizikwa zaidi ya Waislamu 400 wa jamii ya Rohingya suala ambalo linaonyesha maafa ya kutisha na mauaji ya kizazi nchini Myanmar. 
Kutokana na mashinikizo na mbinyo wa serikali ya Myanmar kwa waandishi wa habari, viongozi wa nchi hiyo wamezuia kuakisiwa maafa ya kibinadamu yanayowakabili Waislamu wa Rohingya.
Kuanzia mwaka 2012 wanajeshi wa Myanmar wakishirikiana na mabudha wenye misimamo mikali walianzisha duru mpya ya umwagaji damu na ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya na kwa kuchoma moto ardhi za Waislamu hao wamekuwa wakifuatilia suala la kukitokomeza kizazi cha Waislamu hao katika mkoa wa Rakhine. 
Ni kwa kuzingatia ukweli huo, ndio maana Umoja wa Mataifa una wasiwasi kwamba, hali hiyo huenda ikapelekea kuibuka mapigano ya kikaumu na kikabila nchini Myanmar na mapigano hayo kuvuka mpaka na kuingia katika nchi nyingine na hivyo kushindwa kudhibiti hali ya mambo.
Hali hiyo ndio iliyoufanya Umoja wa Mataifa utoe wito wa kutambulisha haki za kiraia za Waislamu wa Rohingya. 
Stéphane Dujarric msemaji wa Umoja wa Mataifa anasema kuwa: Umoja wa Mataifa unataka Waislamu wa Rohingya wapatiwe haki za kiraia au iweke sheria ambayo itatoa haki ya raia hao kuishi maisha ya kawaida na bila bughudha katika mkoa wa Rakhine.
Kwa kuzingatia kwamba, serikali ya Myanmar imepuuza matakwa ya Umoja wa Mataifa ya kuhitimisha dhulma na ukatili dhidi ya Waislamu wa Rohingya, duru za kimataifa  zinautaka umoja huo na asasi nyingine kama Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) kuchukua hatua na za kivitendo kwa ajili ya kuishinikiza serikali ya nchi hiyo.
Gholamreza Khoshroo, balozi na mwakilishi wa kudumu wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Umoja wa Mataifa anasema: Masaibu ya Waislamu wa Rohingya yanahesabiwa kuwa moja ya mambo ya dharura ya jamii ya kimataifa na kuna haja ya kuchukuliwa hatua za haraka kuhitimisha masaibu hayo. Umoja wa Mataifa nao unapaswa kuingilia suala hilo kupitia Baraza Kuu la umoja huo na asasi nyingine zilizoko chini ya chombo hicho.
Thaung Tun, mshauri wa usalama wa taifa wa serikali ya Myanmar anasema: Sisi tumekuwa tukifanya mashauriano na nchi rafiki ili suala hili lisipelekwe katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. China ni rafiki yetu na tuna uhusiano wa kirafiki pia na Russia, hivyo itawezekana kulifanya jambo hili lifanikiwe.
Ala Kulli haal, suala la mauaji ya kizazi nchini Myanmar ni maudhui ya kimataifa na nchi wanachama wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Matiafa zina jukumu zito kwa ajili ya kukabiliana na jambo hilo. katika upande mwingine, hatua ya serikali ya Myanmar ya kuzitegemea baadhi ya nchi hizo kama China kwa ajili ya kuendelea kufanya mauaji ya kimbari dhidi ya Waislamu wa Rohingya, ni jambo ambalo linaweza kuhairibu haiba ya nchi hizo mbele ya fikra za waliowengi ulimwenguni.
chanzo:parstoday.

Comments