Simba imemaliza duru la kwanza bila kupoteza mchezo katika mechi 15 ilizocheza, lakini katika kuonyesha imepania msimu huu, klabu hiyo imesisitiza kuwa wao bwana hawaachi kitu.
Hesabu zao ni kutaka kumaliza msimu bila kupoteza mchezo na kubeba ndoo waliyoikosa kwa zaidi ya miaka mitano. Simba ilitwaa taji la Ligi Kuu Bara msimu wa 2011-2012.
Vinara hao leo Jumapili inashuka dimbani kuikaribisha Ruvu Shooting ambayo katika miaka minne iliyopita haijawahi kupata hata sare mbele yao.
Ruvu inaingia kwenye mchezo wa leo na presha kubwa baada ya kupoteza mchezo wa mzunguko wa kwanza kwa kipigo cha aibu cha mabao 7-0 mbele ya Simba.
Habari mbaya zaidi kwa Ruvu ni kwamba, yule Emmanuel Okwi aliyewapiga magoli manne mwenyewe, kwa sasa yupo moto akiwa amefunga mabao manne pia katika mechi tatu za mwisho alizoichezea Simba.
Kombinesheni ya Okwi na John Bocco imeshika kasi pia, ikiwa ndiyo pacha hatari zaidi ya ushambuliaji Ligi Kuu Bara baada ya kufunga mabao 19 mpaka sasa.
Simba inaingia kwenye mchezo huo ikiwa na hali ya kujiamini kwani, inaongoza Ligi na pointi 35 wakati Ruvu wapo nafasi ya 12 na pointi 14.
Kocha wa Simba Mfaransa, Pierre Lechantre alisema maandalizi yote yamekwenda vizuri kilichobaki ni wachezaji wake kutimiza yale ambayo amewaelekeza wakiwa mazoezini ili kuhakikisha wanapata pointi tatu jambo ambalo ni muhimu.
“Wachezaji wamefanya vizuri mazoezini. Tulifanya marekebisho katika sehemu ambazo zilikuwa na mapungufu hasa kwenye faulo, kona, kufunga na kuna na baadhi ya mbinu nyingine mpya nilikuwa nikiwapatia. Tumekwenda vizuri sana,” alisema Lechantre.
Kocha Ruvu Shooting Abdulmutik Haji ‘Kiduu’ alisema katika mechi ya kwanza hawakuwa kamili, kwani kuna wachezaji wake saba hawakuwepo kikosini, lakini mechi ya leo wapo kamili na kwa maandalizi ambayo wamefanya wana imani kuwa watamaliza dakika 90 wakiwa washindi.
“Tumefanya usajili mzuri katika dirisha dogo na nimeimarisha safu ya ulinzi ambayo, ilikuwa na mapungufu makubwa na kusababisha kufungwa magoli mengi katika mechi yetu ya kwanza,” alisema Kiduu.
MECHI NYINGINE
Mbali na mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa, hasa kutokana na ukweli watani wa Simba, Yanga jana walipata ushindi muhimu ugenini dhidi ya Lipuli Iringa, lakini viwanja viwili vingine vitawaka moto ukiwamo ule wa Kambarage mjini Shinyanga.
Kwenye uwanja huo mapema mchana, wenyeji Chama la Wana, Stand United itaikaribisha Mtibwa Sugar, huku kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, Mbao FC itaikaribisha Kagera Sugar katika pambano jingine tamu.
Katika mechi zao za duru la kwanza Mbao FC ikiwa ugenini mjini Kaitaba iliinyoa Kagera kwa bao 1-0, ushindi kama iliyoupata Mtibwa dhidi ya Stand United kwenye mashamba ya Manungu, Turiani mkoani Morogoro.
Comments