Bocco, Okwi wawasha mitambo Afrika.

WENYE michuano yao wamerudi. Ndio, Simba jana  Jumapili ilirudi kwa kishindo katika michuano ya Afrika baada ya kuifumua Gendermarie Nationale ya Djibout mabao 4-0, huku Said Ndemla, John Bocco na Emmanuel Okwi wakizidi kung’ara.
Wekundu hao walikuwa nje ya michuano ya Afrika kwa siku 1,806 tangu waliposhiriki mara ya mwisho mwaka 2013, lakini jana walithibitisha kuwa mitambo yao imewaka kwa kupata ushindi huo katika pambano la mkondo wa kwanza wa raundi ya awali ya Kombe la Shirikisho Afrika lililopigwa Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam.
Ushindi huo umeiweka Simba katika nafasi nzuri ya kufuzu raundi ya kwanza ya michuano hiyo inayoweza kuikutanisha na Al Masry ya Misri ambayo juzi Jumamosi iliwafumua Green Buffaloes ya Zambia mabao 4-0 jijini Cairo, Misri.
Mashabiki wa Simba waliofurika kwa wingi uwanjani walikuwa na furaha baada ya kulishuhudia kwa mara ya kwanza chama lao likiamsha dude katika mechi za Afrika tangu walipong’olewa kwa aibu na Recreativo de Libolo ya Angola kwa jumla ya mabao 5-0.
Mechi ya mwisho ya Simba katika michuano ya Afrika ilikuwa Machi 3, 2013 ilipolala 4-0 mjini Calulo, baada ya awali kucharazwa bao 1-0 nyumbani jijini Dar.
NDEMLA ALIAMSHA
Akicheza kwa mara ya kwanza mechi ya kimataifa akiwa na Simba, Said Ndemla, ambaye amekuwa mtamu tangu awe chini ya makocha Masudi Djuma na Mfaransa, Pierre Lechantre, alifunga bao la mapema dakika ya kwanza kwa mpira wa faulo.
Faulo hiyo ilitokana na Bocco kuchezewa vibaya na  beki wa Gendermerie na kupiga kiki iliyoenda wavuni moja kwa moja.
Mabao mengine mawili ya vichwa yaliyofungwa na Bocco katika dakika za 32 na 45 yalitosha kuipeleka Simba mapumziko ikiwa mbele 3-0.
Bao la kwanza la Bocco lililokuwa la pili kwa Simba alilifunga katika piga nikupige baada ya Kichuya kupiga krosi, huku lile jingine sekunde chache kabla ya mapumziko aliunganisha krosi ya Okwi.
Katika kipindi hicho cha kwanza Simba ilitawala mchezo kwa kufanya mashambulizi mengi langoni mwa Wadjibout walioonekana wazi kuwa wepesi japo walifanya mashambulizi ya kushtukiza yaliyozimwa na mabeki wa Simba.
Timu hiyo pia ilipoteza penalti ya dakika ya 50 iliyopanguliwa na kipa, Aishi Manula. 
OKWI KAMA KAWA
Emmanuel Okwi ambaye alikosa mabao mengi ya wazi katika kipindi cha kwanza aliihakikisha Simba ushindi kwa kutupia nyavuni bao la nne dakika za jioni kabisa na kuwafanya Wekundu hao kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu raundi ya pili.
Hilo ni bao la 14 kwa Okwi msimu huu kwa mashindano yote akiichezea Simba, 13 yakiwa ya Ligi Kuu Bara na yote akiyafunga viwanja vya jijini Dar es Salaam.
MZEE MWINYI AFUTA USEMI
Aliyekuwa mgeni rasmi wa pambano hilo, Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaj Ali Hassan Mwinyi, amesema kwa ushindi huo wa kishindo wa Simba amefuta usemi wake kuwa Tanzania ni Kichwa cha Mwendawazimu, alioutoa miaka ya nyuma.
“Simba imecheza vizuri, nimeona mpira safi ambao kwa hakika walistahili kunialika leo hapa na kwa matokeo haya nafuta kauli yangu ya Kichwa cha Mwendawazimu. Niwapongeze Simba kwa ushindi huu,” alisema Alhaji Mwinyi.
MAKOCHA WANENA
Kocha Msaidizi wa Simba, Masudi Djuma, alisema wanamshukuru Mungu kwa matokeo ya ushindi nyumbani, kwani imewaweka katika nafasi nzuri kwa mchezo wa marudiano na kwa sasa wanaelekeza nguvu katika Ligi Kuu Bara.
“Tulicheza kwa tahadhari kwani tuna mechi nyingi ambazo zote zina umuhimu, lakini tunashukuru kwa ushindi huu wa mabao manne. Vijana walicheza vizuri,” alisema Djuma.
Naye Kocha wa Gendermarie, Mvuyekule Issa, alisema kipigo hicho hakijawashtua sana kwani vijana wake ni chipukizi na wamecheza na timu kubwa.


“Bado naamini tunaweza kupata matokeo mazuri nyumbani, kama tukitolewa tutajipanga upya,” alisema.

Comments