Amri ya Trump ya kuendelea shughuli za gereza linalonuka kwa ubaya la Guantanamo.

Amri ya Trump ya kuendelea shughuli za gereza linalonuka kwa ubaya la GuantanamoBaada ya kupita masaa machache tu tangu Donald Trump atoe hotuba yake ya kila mwaka mbele ya Kongresi, rais huyo wa Marekani ametoa amri jela inayonuka kwa ubaya ya Guantanamo iendelee na shughuli zake.

Amri hiyo ya Trump inaitaka Wizara ya Ulinzi ya Marekani Pentagon ihakikishe watu wanaoshukiwa kuhusika na vitendo vya ugaidi wanawekwa kwenye kambi ya X-Ray iliyoko kwenye ghuba ya Guantanamo ya Cuba na kuandaa mazingira ya kuwafungulia mashtaka katika mahakama za kijeshi. 
Kabla ya kutoa amri hiyo, Trump alisema katika hotuba ya kila mwaka aliyotoa mbele ya Kongresi: 
"Tulifanya ujinga huko nyuma kuwaachia huru mamia ya magaidi hatari mpaka tumekuja kushuhudia tunakabiliana nao tena katika medani ya mapambano; ni magaidi mbalimbali akiwemo kiongozi wa Daesh Abubakar Al Baghdadi". 
Trump aidha ameitaka Pentagon ifikirie kutumia "kila wenzo" kwa ajili ya kupambana na magaidi. 
Huo "kila wenzo" aliokusudia unaweza kuwa ni pamoja na kuwaweka kizuizini watu kwa kipindi kirefu pasi na kuwasomea mashtaka, kuwatupa korokoroni kwenye jela kama ya Guantanamo na kuwatesa na kuwaadhibu washukiwa kwa anuai za mateso na adhabu ikiwemo kuwazuia kupumua kwa kuwamiminia maji. Kwa maneno mengine, ni kupuuza na kukanyaga waziwazi haki za binadamu.
Dokta Homer Venters wa Jumuiya ya Madaktari Wasio na Mipaka anasema: "Jela ya Guantanamo imejulikana dunia nzima kuwa nembo ya utesaji na utovu wa uadilifu wa Marekani, ikiwa ni dhihirisho la mfumo usio wa kisheria, usio wa kimaadili na wenye madhara, wa kuwaweka kizuizini watu kwa muda usiojulikana; na inapasa ifungwe mara moja".
Bila ya shaka hata kabla ya Trump kuingia madarakani, gereza la Guantanamo lilikuwa likiendelea kuwashikilia makumi ya washukiwa wa ugaidi. 
Ukweli ni kwamba ahadi aliyokuwa ameitoa Barack Obama, rais wa Marekani aliyetangulia, ya kuifunga jela hiyo inayonuka kwa ubaya mwaka mmoja baada ya kuingia Ikulu ya White House haikutimizwa. 
Katika kipindi chote cha miaka minane ya urais wa Obama, wabunge wa chama cha Republican walitumia njia mbalimbali kuzuia kufungwa jela hiyo, ikiwemo kukataa kutengwa bajeti kwa ajili ya kushughulikia ufungaji wake au kupinga kuhamishiwa wafungwa wa jela hiyo kwenye maeneo mbalimbali ndani ya Marekani.
Yote hayo yamejiri katika hali ambayo, kwa muda wote wa miaka 15 tangu gereza la Guantanamo lianze shughuli zake, jumuiya tofauti za kimataifa na makundi mbalimbali ya kutetea haki za binadamu yamekuwa yakitamka bayana kuwa yanayofanywa ndani ya jela hiyo yanakinzana dhahiri shahiri na misingi ya haki za binadamu na haki za msingi za watu wanaoshikiliwa humo, ikiwemo haki ya kubainishiwa makosa  na mashtaka yanayowakabili, haki ya kupatiwa mahakama stahiki za kusikiliza kesi zao na haki ya kulalamikia mazingira ya kutisha na yasiyovumilika ya ndani ya jela hiyo.
Hivi sasa pia rais wa sasa wa Marekani ametilia mkazo tena kuendelea shughuli za jela ya Guantanamo kupitia hatua ya kimaonyesho yenye lengo la kuonyesha kuwa Washington imeazimia kwa dhati kukabiliana na ugaidi wa kimataifa. 
Pamoja na hayo, kitu muhimu zaidi kuhusiana na kuendelea shughuli za gereza la Guantanamo ni kurejea tena Marekani katika kipindi hiki cha urais wa Donald Trump kwenye enzi za ukiukaji wa wazi wa haki za binadamu, kuwatesa washukiwa wa masuala ya kiusalama na kuyafufua tena masuala kama utesaji wa kutumia mbinu ya kukosesha kupumua kwa kumimina maji, kuanzisha jela za kutisha katika pembe mbali mbali za dunia na safari za anga za kuhamishia wafungwa kutoka sehemu moja hadi nyengine.
 chanzo:parstoday.

Comments