Taarifa ya jeshi la Afrika Kusini imesema kuwa, iwapo uchunguzi huo utabaini kwamba ni kweli wanajeshi wa nchi hiyo wamewadhulumu raia wa Kongo DR, basi watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Jana Jumatatu, Stephane Dujarric, msemaji wa Umoja wa Mataifa alisema Kikosi cha Kulinda Amani cha umoja huo nchini Kongo MONUSCO kimepokea malalamiko manne kutoka kwa wakazi wanne wa mashariki mwa Kongo, wanaodai kunyanyaswa na baadhi ya askari wa Afrika Kusini, ambao ni miongoni mwa askari elfu moja wa nchi hiyo kwenye kikosi cha MONUSCO.
Askari hao wa Afrika Kusini wanatuhumiwa kuwanyanyasa kingono wakazi wa eneo hilo wakiwemo watoto wadogo, miongoni mwa dhulma zingine.
UN imeipa Afrika Kusini siku 90 kukamilisha uchunguzi wake kuhusiana na ukiukaji huo wa haki za binadamu na kisha kuikabidhi ripoti.
Lambert Mende, msemaji wa serikali ya DRC amesema inagawaje hana habari yoyote kuhusu madai hayo ya unyanyasaji, lakini uchunguzi kuhusu kadhia hiyo utafanywa na Afrika Kusini na wala sio maafisa wa serikali ya nchi hiyo.
chanzo:parstoday.
Comments