Wasiwasi wa asasi za kimataifa wa kushadidi vitendo vya utumiaji mabavu vya Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina.
Utawala haramu wa Israel chini ya kivuli cha uungaji mkono wa madola ya Magharibi ulikamilisha mwaka uliopita wa 2017 kwa jinai zake dhidi ya Wapalestina bila ya wasiwasi wowote.
Katika uwanja huo, Harakati ya Kimataifa ya Kutetea Haki za Watoto Tawi la Palestina imetangaza kuwa: Katika mwaka uliomalizika wa 2017, wanajeshi wa Israel waliwaua shahidi watoto 15 wa Kipalestina katika Ukanda wa Gaza, Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan na Quds Tukufu. Hivi karibuni duru za habari zilitoa taarifa zikikiri kwamba, kuanzia mwaka 2000 hadi Februari mwaka jana, watoto 2,069 wa Kipalestina waliuawa shahidi kufuatia mashambulio ya wanajeshi vamizi wa Israel.
Riyadh Ashqar, msemaji wa kituo cha utafiti wa masuala ya mateka wa Kipalestina naye ametangaza kuwa: Katika mwaka uliopita wa 2017, mamia ya wanawake na watoto wa Kipalestina walitiwa mbaroni na wanajeshi wa Israel.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa pia ameelezea wasiwasi mkubwa alionao kutokana na kuendelea kushikiliwa mabinti wadogo wa Kipalestina katika magereza ya utawala ghasibu wa Israel.
Duru za habari zimetangaza kuwa, maafisa wa ngazi za juu wa Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa UNICEF pamoja na asasi zisizo za kiserikali zinazotetea haki za watoto zimo mbioni kushirikiana ili kuandaa uwanja wa kutiwa jina la Israel katika orodha ya wakiukaji wa haki za watoto kutokana na utumiaji mabavu mkubwa wa utawala huo ghasibu dhidi ya watoto wa Kipalestina.
Licha ya kuwa, jumuiya za kimataifa ambazo kutokana na mashinikizo ya madola ya Magharibi hususan Marekani kikawaida hunyamazia kimya jinai za utawala dhalimu wa Israel, lakini radiamali kubwa ya hivi karibuni ya asasi hizo dhidi ya jinai za Israel na ukwamishaji mambo wa utawala huo bandia kwa shughuli za asasi hizo ni jambo la kutaamaliwa na kutiliwa maanani.
Ripoti mbalimbali zimetolewa katika miaka ya hivi karibuni ambazo zinaonyesha juu ya kuweko muamala usio wa kibinadamu na wa utumiaji mabavu wa utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina. Hii ni katika hali ambayo, hadi sasa Umoja wa Mataifa haujachukua hatua yoyote ya maana dhidi ya ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu unaofanywa kila uchao na Israel.
Fikra za waliowengi ulimwenguni zimekuwa zikiulaani utawala unaotenda jinai wa Israel na hivyo kuonyesha chuki na hasira zao kwa utawala huo ambao kutokana na utumiaji mabavu na mauaji dhidi ya watoto wa Kipalestina unatambuliwa kuwa, "Muuaji wa Watoto".
Kimsingi Israel iko katika kilele cha tawala ambazo zimekuwa zikiwatia mbaroni watoto wadogo, kuwafunga jela na kuwatesa suala ambalo linakinzana waziwazi na sheria za kimataifa.
Kwa hakika miamala ya ukandamizaji ya jeshi la Israel dhidi ya watoto wa Kipalestina inakinzana bayana na hati ya pande nne ya Geneva Uswisi ambayo inasisitiza juu ya kuheshimiwa haki za wananchi ambao ardhi yao imekaliwa kwa mabavu hususan kulindwa na kuheshimiwa haki za watoto.
Pamoja na hayo na licha ya matakwa ya kila upande ya walimwengu ya kuliweka jina la Israel katika orodha ya tawala zinazokiuka na kukanyaga haki za watoto duniani, Umoja wa Mataifa unakwepa kufanya hivyo. Hatua hiyo ya Umoja wa Mataifa imeendelea kuandaa uwanja wa kuendelea jinai za Israel dhidi ya Wapalestina hususan watoto wadogo wa ardhi hizo zinazokaliwa kwa mabavu.
Hii ni katika hali ambayo, licha yya kuwa watoto wa Kipalestina kimsingi wanaunda asilimia kubwa ya wahanga wa jinai za Israel wakati wa kujiri mashambulio ya kinyama ya utawala huo ghasibu katika maeneo mbalimbali ya Wapalestina, lakini madola ya Magharibi ambayo siku zote yanadai kuwa ni watetezi wa haki za binadamu, yameendelea kunyamazia kimya jinai hizo za Israel kama vile hakuna kitu chochote cha ajabu kinachotokea huko Palestina.
chanzo:parstoday
Comments